Serikali imesema kuwa Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari unatoa fursa kwa wanahabari mbalimbali kuwa na Haki ya kupata Bima ya Afya kwa ajili ya kupata matibabu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji wa Serikali Bw. Hassan Abbas alipokuwa akizungumza katika kituo cha Redio E Fm kilichopo Jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa Muswada huu utatoa fursa kwa wanahabari kupata Bima ya Afya na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa fedha ya matibabu .
“Muswada huu utasaidia wanahabari kuwa na Bima ya Afya itakayosaidia kupata huduma ya kiafya na kuacha utaratibu ulipo sasa wa kutoa michango wakati mwanahabari anapokuwa mgonjwa au anapofariki.” Alisema Bw. Abbas.
Aidha Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Sehemu ya tatu ya Muswada huu unaeleza kuwa kutakuwa na Mfuko kwa ajili ya Habari ambao lengo lake kuu ni kuwezesha mafunzo kwa wanataaluma ya habari pamoja na kukuza na kuendeleza utafiti na maendeleo katika nyanja ya Habari na Mawasiliano ya Umma.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo ametoa rai kwa wadau na wanatasnia kwa ujumla kuusoma Muswada huu na kutoa maoni yao ambayo yatasaidia kuuboresha ili uweze kutumika kwa ajili ya maendeleo ya Tasnia ya Habari.
“Naomba wadau muusome Muswada huu muuelewe na muweze kutoa maoni yenu kabla haujapelekwa Bungeni kwa mara ya pili ili tasnia hii iwe na hadhi kama inavyostahili.” Aliongeza Bw Abbas.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 upo katika hatua ya kujadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na wadau kutoa maoni kwa ajili ya kuuboresha Muswada huo kabla ya kuwasilishwa Bungeni kujadiliwa.
No comments:
Post a Comment