Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko (katikati), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo, wakati akitoa taarifa kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu. Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Muitikio ya Kitaifa, Dk.Hafidhi Amri, Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tacaids, Elizabeth Kaganda na Mkurugenzi wa Habari na Ulaghibishi, Jumanne Issango.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko (kushoto), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo. Kulia ni Mkurugenzi wa Habari na Ulaghibishi, Jumanne Issango.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Wapiga picha wakichukua taarifa hiyo.
Wanahabari wakiwa kazini.
Na Dotto Mwaibale
MAAMBUKIZO Mapya ya VVU na Ukimwi yameshuka nchini kwa zaidi ya asilimia 20 kati ya mwaka 2010 na 2015 imefahamika.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu.
Alisema maambukizo mapya ya VVU yaliyokadiriwa kuwa watu milioni 2.1 kwa mwaka 2015 Duniani kote wakati maambukizo mapya yameshuka kwa asilimia 50 miongoni mwa watoto duniani.
Alisema watoto 290,000 wapya waliambukizwa mwaka 2010 na watoto 150,000 waliambukizwa mwaka 2015 ambapo maambukizo mapya kwa watu wazima hayajashuka tangu 2010 duniani.
Katika hatua nyingine Dk. Maboko alisema Tafiti zimeonesha kuwa wanawake ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya VVU kwa upande wa Tanzania Bara ukilinganisha na wanaume.
Alisema maambukizo VVU kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 5.3 wanawake wakionesha kuathirika zaidi kwa asilimia 6.2 ukilinganisha na wanaume ambao ni asilimia 3.8.
“Katika utafiti huo wa mwaka 2011 na 2012 ulionyesha kuwa Mkoa wa Njombe ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizo ukiwa na asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mbeya kwa asilimia 9″ alisema Dk.Maboko.
Dk.Maboko alisema Mkoa wa Manyara ulikuwa na kiwango kidogo cha maambukizo ya asilimia 1.5 lakini takwimu za ndani ya mkoa huo eneo la Mirelani kwenye mgodi wa Tanzanite maambukizo ya VVU yalikuwa ni asilimia 16 kiwango ambacho ni cha juu ya Mkoa wa Njombe.
Dk. Maboko aliwaomba wananchi kote walipo kutobweteka kwa mafanikio yaliyo ya mapambano dhidhi ya VVU na ukimwi na kuwa yawe endelevu hata katika maeneo au mikoa ambako kuna maambukizo kidogo ya VVU.
Alisema kama nchi tunatakiwa kuweka nguvu nyingi kifedha na kimkakati katika maeneo na makundi yenye kiwango kikubwa cha maambukizo ya VVU ikiwa ni pamoja na kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za VVU na Ukimwi ili tuendelee kubaini na kupanga mipango dhidi ya ugonjwa huo inayoongozwa na takwimu.
Aliongeza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi (UNAIDS) limeweka malengo ya muda wa kati ya tisini tatu (90-90-90). 90 ya kwanza ikimaanisha asilimia tisini ya watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua hali zao na 90 ya pili ikimaanisha kuwa asilimia tisini ya waliobainika kuwa na VVU kuanza kutumia dawa za kupunguza makali
ya VVU (ARV) mara moja na 90 ya tatu ya walioanza dawa waweze kuwa na ufubazo endelevu wa virusi vya ukimwi mwilini mwao.
Dk. Maboko alitoa mwito kwa wananchi, Taasisi za kijamii, Serikali, watu binafsi na makampuni ya kibiashara kuchangia mfuko wa udhamini wa masuala ya ukimwi (AIDS TRUST FUND-ATF) ulioanzishwa na serikali ili kuondokana na utegemezi kwa wafadhili.
No comments:
Post a Comment