Habari
Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP) umefanya mjadala wa kupinga ukatili katika kata za Kipunguni,Kivule na Mzinga ikiwa ni muendelezo wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika jimbo la Ukonga, yenye kaulimbiu ya “Funguka, Pinga Ukatili wa Kijinsia Elimu Salama kwa Wote”
Akizungumza katika mjadala huo uliofanyika katika kata ya Kipunguni B Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam Afisa wa Program Harakati na Ujenzi wa Nguvu za Pamoja wa Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP) Anna Sangai ameeleza kuwa suala la Ukeketaji ni suala mtambuka linalohitaji kupigiwa kelele kwa nguvu zote na watu wapatiwe elimu waelimike na wawe wanatoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wasikiapo kuna vitendo vya ukatili wa kijinsia kama ukeketaji, na kufafanua kuwa madhara ya ukeketaji ni makubwa kwani humpelekea msichana kuathirika kisaikolojia, kupata maumivu makali,kuuguza kidonda, maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI, kutokwa damu kwa wingi, maradhi ya Fistula na huenda akafariki dunia.
Pia Afisa huyo amewataka polisi kutoa msaada pindi wanapoletewa taarifa za ukatili wa kijinsia kwani kumekuwepo na malalamiko kuwa wamekuwa wakipuuzia pindi wanapoletewa taariza hizo.
Huku Muwezeshaji Mshauri TGNP Agnes Lukanga ameeleza kuwa takribani ya wasichana 4000 wamekeketwa kwa mwaka huu, hivyo ni vyema kila mmoja kujithamini ana nafasi gani kuleta mabadiliko kuhusu ukatili huo unaendele kwa baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo Dodoma, Moshi, Arusha, na Tarime.
Kwa upande wake mwanaharakati Fatuma Abdulrahman ameeleza kuwa ni vyema wazee wa mila kwa makabila yanayofanya vitendo hivyo wapewe elimu ya kutosha kwani wananguvu ya ushawishi huku mwanaharakati mwingine Selemani Mpagazi akisisitiza elimu itolewe juu ya mila potofu na kasumba ya kusema usipo keketwa huolewi iondoke kwa makabila yanayofanya vitendo hivyo, huku wachangiaji wengine wakiwataka wazazi wa kiume na wakike washirikiane kwa pamoja katika mapambano ya ukatili wa kijinsia kwani bila wao hakuna mtoto atakaye keketwa au kufanyiwa ukatili wowote.
No comments:
Post a Comment