• Breaking News

    ..

    ..

    Friday, 16 December 2016

    VYAMA SHIRIKI UCHAGUZI MDOGO ZNZ VYATAKIWA KUZINGATIA SHERIA

    TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa na wagombea watakaoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Dimani visiwani Zanzibar kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ili uchaguzi huo uwe huru na wa haki na kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

    Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alipozungumza na viongozi 19 wa vyama vya siasa waliohudhuria mkutano wa maandalizi ya kufanikisha uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani, Januari 22, mwakani.

    Aliwataka waliohudhuria mkutano huo kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati wa kampeni za vyama vyao zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni pia kutoa ushirikiano kwa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi huo.

    “Ni matarajio ya Tume kuwa, vyama vya siasa vitatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha uchaguzi wetu katika jimbo la Dimani unakuwa huru na wa haki, lengo hili litafanikiwa tu iwapo vyama na wagombea wote watazingatia na kufuata sheria na maelekezo na maadili ya Tume,” alisema Jaji Lubuva.

    Amevitaka vyama vyote vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo wakati wa kampeni vijikite katika kuelezea sera zao na si vinginevyo na kuepuka matumizi ya lugha zinazoweza kusababisha machafuko.

    Alisema katika kufanikisha uchaguzi huo, kila chama cha siasa kina haki ya kuteua wakala mmoja kwa kila kituo cha kupigia kura ili kuongeza uwazi katika uchaguzi huo na kuongeza kuwa mawakala hao watapangwa kwenye vituo vilivyo ndani ya Shehia wanakoishi ili waweze kuwatambua wapiga kura katika eneo husika.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI