Wakati serikali ikiendelea kupambana na tatizo la vifo vya kina mama na watoto, ambapo kwa mujibu wa takwimu ya wizara ya afya inaonyesha kuwa kati ya vizazi hai laki moja kunatokea vifo 432 kila mwaka.
Shirika la Afya Duniani (WHO) Disemba 14, 2016 limetoa msaada wa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) 50 huku Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) likitoa magari ya kuratibu afya ya mama na mtoto 8 kwa ajili ya kuongeza nguvu za mapambano ya kutokomeza vifo vya kina mama na watoto nchini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya baaadhi ya magari hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema magari hayo yatagawiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kutokana kwamba mikoa hiyo inaongoza kwa vifo vya kina mama na watoto kwa sababu ya kukosekana kwa huduma bora za afya, miundombinu bora hasa barabara pamoja na uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa.
"Wizara imepokea magari 50 ambayo yatagawiwa katika kila jimbo, tumechagua kuyapeleka katika mikoa ya Kanda ya ziwa kwa sababu tulifanya tathimini na kubaini kuwa ina changamoto kubwa ya vifo vya kina mama na watoto," amesema.
Sambamba na hilo, Ummy amesema wizara yake imeanza mkakati wa miaka minne wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 30, na kwamba ifikapo 2020 vifo hivyo vipungue kutoka 432 kati ya vizazi hai 100,000 na kufikia 392.
Baada ya kukabidhi magari hayo kwa baadhi ya wabunge wa mikoa ya Kanda ya Ziwa , Waziri wa Afya, Ummy amewataka Waganga Wakuu, Wakurugenzi na Wabunge wa mikoa hiyo kuyasimamia magari hayo.
Hata hivyo, Mbunge wa Kwimba Richard Ndassa ameishukuru serikali kwa kuuratibu mpango huo kwa kuwa magari hayo yatasadia mkakati kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Pia, ameiomba Wizara ya Afya kujenga vituo vya afya katika kila kijiji na kata ili wananchi wapate huduma hiyo karibu.
No comments:
Post a Comment