Na Issa Bwana
TIMU ya Azam FC itamenyana na Taifa Jang’ombe katika Nusu Fainali ya kwanza Kombe la Mapinduzi Jumanne jioni Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hiyo inafuatia Taifa kuwalaza waliokuwa mabingwa watetezi, URA ya Uganda 1-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi A usiku huu Uwanja wa Amaan.
Bao pekee la Taifa Jang’ombe limefungwa na Mohammed Said kwa penalti, baada ya Ally Badru kuangushwa kwenye boksi. Mapema URA nao walipoteza penalti baada ya Bogota Labama kuangushwa kwene boksi.
Nusu Fainali ya Pili itawakutanisha watani wa jadi, Simba na Yanga Jumanne Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Hiyo inafuatia Simba SC kushinda 2-0 dhidi ya Jang’ombe Boys jioni ya leo katika mchezo wa mwingine wa Kundi A.
Matokeo hayo yanaifanya Simba imalize kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake 10, ikifuatiwa na Taifa Jang’ombe pointi tisa, Jang’ombe Boys pointi sita na URA pointi nne.
Ikumbukwe Yanga imeshika nafasi ya pili Kundi B nyuma ya Azam walioongoza kwa wastani wa mabao baada ya kufungana kwa pinti saba kila timu.
Mabao yote ya Simba SC leo yamefungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo moja kila kipindi.
No comments:
Post a Comment