• Breaking News

    ..

    ..

    Friday, 6 January 2017

    SIHABA HAJI VUAI:AMEWATAKA MAOFISA KUFANYAKAZI KWA KUFUATA RATIBA ZINAZOTAMBULIKA KISHERIA,ILI KURAHISISHA UTENDAJI WA SHUGHULI ZAO VISIWANI PEMBA


    wete               Na.Masanja Mabula-Pemba                                                                                          

    Ofisa Mdhamin aliyasema hayo katika mkutano na maofisa hao, huko Chamanangwe, Wilaya ya Wete wakati alipokuwa akiwaelekeza utaratibu wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma.
    Alisema kuwa, watumishi wa umma ni lazima watekeleze shuguli zao kwa utaratibu maalum unaotambulika na wanajamii anaowatumikia jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa matatizo yanayoweza kujitokeza.
    Sambamba na hayo aliwataka watumishi hao, kutoa taarifa kwa wakati zinapotokezea zarura za kutofika katika eneo la kazi, ili kusaidia urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa uhakika.
    Akitaja vipengele muhimu kwa maofisa wilaya alisema kuwa, ni kusimamia watendaji ndani ya Wilaya, kusimamaia utekelezaji wa sheria ya sekta yao, kutoa elimu na utaalamu walionao kwa kushirikiana na Wilaya, kusimamia maendeleo ya sekta wanayoifanyia kazi ndani ya Wilaya kupitia miradi inayotekelezwa pamoja na kuunganisha taasisi wanazozifanyia kazi na Wilaya husika.
    ‘’Wadau wa sekta yetu wanahitaji kufuatiliwa na kupatiwa ushauri wa kitaalamu kila hatua katika shughuli zao, lazima mpite, malalamiko yamekuwa mengi wanasema hawapitiwi kwa kweli ni tatizo ufanisi hautapatikana’’, Ofisa Mdhamin alieleza.
    Hata hivyo aliwasisitiza, watumishi hao, kufanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na sekta nyengine za Serikali jambo ambalo litasaidia kupata mafanikio katika kazi zao, huku akiwaahidi kuyafanyia kazi matatizo yanayorejesha nyuma juhudi zao hatua kwa hatua kila hali itakaporuhusu.
    Wakichangia katika mkutano huo, maofisa hao, walisema kuwa, sambamba na ufuataji wa ratiba wamekuwa wakikwazwa na usafiri wa kufikia katika maeneo kwa wakati unaohitajika.
    ‘’Kwa kweli muheshimiwa kazi tulizonazo ni nyingi na tunajitahidi kadri tunavyoweza kuhakikisha tunatekeleza wajibu, lakini mara nyingi kilio chetu ni usafiri, vyombo ni kidogo wakati mwengine tunathubutu hata kuazima kwa watu nje ya ofisi, ni tatizo,’’ alisema Ali Abdi Othman, ambae ni Ofisa Misitu Wilaya ya Mkoani.
    Kwa upande wake, Ofisa Mifugo Wilaya ya  Mkoani, Abdalla Hamad Khamis, alisema kuwa ni vigumu kufuata ratiba katika utekeleaji wa shughuli za mifugo kutokana na muingilianao wa matukio katika maeneo tofauti.
    Alisema, pamoja na utekelezaji wa shughuli za ushauri na uzalishaji wa mifugo katika maeneo yao, wakati mwengine huwalazimu kufanyakazi katika maeneo yasiokuwa ya kwao kikanda na hata kiwilaya kutegemea na ukubwa wa tatizo linapojitokeza.
     ‘’Bosi kwa kweli kufuata ratiba itakuwa ngumu, maana kila muda tumekuwa tukipokea simu za matukio mbali mbali, hivyo unapopanga kwenda kufanyakazi mara nyingi sivyo inavyokuwa kwa siku,’’alisema Ofisa huyo.
    Kwa upande wake, Ofisa Uvuvi Wilaya ya Micheweni, Mzume Juma Faki, aliwataka maofisa wenzake kuongeza bidii ya kazi kwa kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli zao, ili kwenda sambamba na maagizo ya utumishi kwa umma.
    Sambamba na hilo, alisema kuwa ushirikiano wa kazi ni nguzo moja wapo itakayowawezesha kufikia malengo kutoka hatua moja kwenda hatua nyengine, na hivyo kupelekea kueleweka vyema katika jamii wanazozitumikia.
    Nae Ofisa Mkuu wa Uendeshaji na Utumishi, Issa Nassor Bakar, aliwataka watumishi hao kuwatumikia wanajamii kwa moyo mmoja kwa kufuta taratibu na kanuni za kisheria, ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
    Alisema, muda umefika wa kuleta mabadiliko ndani ya jamii kwa kuachana na tabia ya  kufanya kazi kwa mazoea ambayo hupoteza muelekeo wa malengo ya Serikali kiujumla.
    ‘’Lazima mubadilike, mfanye kazi tena mjitahidi, na sheria na kanuni zipo, mnatakiwa kuziheshimu na kuzifuata kama inavyotakiwa,’’alisema Issa , Mkuu wa Uendeshaji na Utumishi.
    Aidha, alisema kuwa, Serikali kupitia watumishi wa umma inategemea maendeleo ya shughuli za taasisi kwa ushirikiano wa moja kwa moja na jamii.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI