Na Issa Bwana, ZANZIBAR
HATUA ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inatarajiwa kuhitimishwa leo kwa michezo miwili ya Kundi A, ambayo itaamua timu za kwenda Nusu Fainali.
Hadi sasa hakuna timu yenye uhakika wa Nusu Fainali katika Kundi hilo, ikiwa URA inaweza kufikisha pointi saba za Simba na Jang’ombe Boys na Taifa Jang’ombe wote wanaweza kumaliza na pointi tisa.
Simba itacheza mechi ya kwanza leo dhidi ya Jang'ombe Boys kuanzia Saa 10:00 jioni, wakati mabingwa watetezi, URA kutoka Uganda, wataingia katika mchezo wa pili dhidi ya Taifa Jang'ombe kuanzia Saa 2:30 usiku.
Japokuwa inaongoza Kundi A kwa sasa, lakini Simba SC inaweza kujikuta inafungasha virago kurejea Dar es Salaam iwapo tu itafungwa leo.
Ushindi utawafanya wapinzani wao wafikishe pointi tisa na matokeo yoyote ya mchezo wa usiku yasiweze kuinusuru Simba kubaki kwenye mashindano.
Mechi ya usiku ikiisha kwa sare Taifa itafikisha pointi saba, hivyo timu ya kuungana na Jang’ombe Boys (kama itashinda) itatazamwa kwa wastani wa mabao. Hata URA wakishinda, watafikisha pointi saba na maana yake timu ya kuungana na Jang’ombe Boys itatafutwa kwa wastani wa mabao.
Ni mbaya zaidi ikiwa baada ya Simba kupoteza mechi kwa Jang’ombe Boys na Taifa Jang’ombe itashinda pia. Wazi Simba wanaingia katika mchezo mgumu leo, ambao watahitaji japo sare ili kuwapunguza Jang’ombe Boys.
Tayari kocha wa Simba SC, Mcameroon Joseph Marius Omog amekwishasema kwamba anatarajia upinzani mkali leo kutoka kwa Jang’ombe Boys.
Omog alisema kwamba Jang’ombe Boys ni timu nzuri na ilidhihirisha hilo baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, URA 2-1, hivyo hata mbele ya Simba watakuwa tishio tu.
Kwa sababu hiyo, Omog amesema kwamba amewandaa vizuri vijana wake kwenda kucheza kwa tahadhari ili kuepuka kuingia kwenye mitego ya Jang’ombe Boys.
“Utakuwa mchezo mgumu. Hiyo timu (Jang’ombe Boys) imewafunga wanaoshikilia Kombe, imefunga timu nzuri ambayo sisi tumetoka nayo sare, kwa huyo tunauelekea mchezo mgumu na tutacheza kwa tahadhari tupate matokeo mazuri twende Nusu Fainali,”alisema Omog.
Simba SC inaongoza Kundi A kwa pointi zake saba, baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Taifa Jang’ombe, 1-0 dhidi ya KVZ na sare ya 0-0 na URA. Jang’ombe Boys wanafuatia kwa pointi zao sita, mbele ya URA yenye pointi nne na Taifa pointi tatu.
Mechi za mwisho za Kundi B zilichezwa jana Zimamoto ikiifunga Jamhuri 2-0 na Azam ikiilaza Yanga 4-0, wakati Nusu Fainali zinatarajiwa kuchezwa Januari 10 na Fainali Januari 13, mwaka 2017
No comments:
Post a Comment