• Breaking News

    ..

    ..

    Monday, 9 January 2017

    TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA

    posi
    posiJeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-
    KUPATIKANA NA SILAHA [GOBOLE]
    Mnamo tarehe 07.01.2017 majira ya saa 16:30 jioni huko katika Kijiji cha Mhwela, Kata ya Mswiswi, Tarafa ya Ilongo iliyopo mpakani mwa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi na Mbarali Mkoa wa Mbeya, askari Polisi wakiwa katika msako walimkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JOHN NOAH [28] mkazi wa Ilongo akiwa na silaha aina ya gobole yenye namba MB 2688 iliyokuwa imefukiwa kwenye shamba la migomba ambayo alikuwa anamiliki kinyume cha sheria. Upelelezi unaendelea.
    Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Kumekuwa na matukio 03 ya mauaji kama ifuatavyo:-
    Mnamo tarehe 07.01.2017 majira ya saa 12:30 mchana huko Kijiji na Kata ya Ifumbo, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi waliofahamika kwa majina ya 1.  PASCHAL SIMCHIMBA [29] Mkazi Kanga na 2. TEGEMEA HENUS [34] Mkazi wa Tete waliuawa na wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi baada ya kuvamia eneo la wachimbaji wadogo wa dhahabu wakiwa na silaha aina ya Short gun iliyotengenezwa kienyeji kwa lengo la kufanya unyang’anyi na ndipo walizidiwa nguvu na wananchi hao.
    Inadaiwa kuwa majambazi hao walikuwa watano huku wakiwa na silaha silaha aina ya short gun iliyotengenezwa kienyeji ikiwa imekatwa  mtutu  na risasi mbili ndani ya magazini. Aidha inadaiwa kuwa wakati wa tukio hilo risasi zilizogoma kupiga ndipo walizidiwa nguvu na wananchi kisha kupigwa mawe hadi kufa na kuchomwa moto.
    Chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali katika kitongoji cha Kasangakanyika ambalo wachimbaji wadogo hufanya shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu. Marehemu wote wawili walishawahi kushitakiwa na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha  mwaka 2013 na kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30. Pia watuhumiwa hao walikata rufaa na kuachiwa mwaka 2014. Watuhumiwa watatu walikimbia mara baada ya tukio hilo juhudi za kuwatafuta zinaendelea.
    Mnamo tarehe 07.01.2017 majira ya saa 09:00 asubuhi huko katika Kijiji cha Dimbwe kilichopo Kata ya Ulembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Kipolilsi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la VARENCY POSTA [25] mkazi wa kijiji cha Dimbwe alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Ilembo baada ya kuchomwa kitu chenye ncha kali kichwani na mtu aliyefahamika kwa jina la MISIS EDWARD [33] mkazi wa Dimbwe.
    Inadaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kutokana na binti wa Mtuhumiwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu. Inadaiwa kuwa mtuhumiwa kabla ya kutenda kosa hilo alimvizia njiani marehemu akiwa anatoka kuangalia mpira na kisha kumchoma kitu chenye ncha kali hali iliyosababisha kutokwa damu nyingi na kupelekea kifo chake akiwa anapatiwa matibabu. Mtuhumiwa amekamatwa. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
    Mnamo tarehe 07.01.2017 majira ya saa 08:00 asubuhi huko Kijiji cha Ngolela, Kata ya Ipinda, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NURU ROMAN @ MWANG’OLELA [35] Mkazi wa Ubaruku Wilaya ya Mbarali na mwenyeji wa Bujela Kisale Wilaya ya Kyela aliuawa kwa kupigwa mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa tuhuma za wizi.
    Katika tukio hilo EDWIN SHURIMA [40] mkazi wa Ubaruku Mbarali ambaye alikuwa na marehemu alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kyela na hali yake inaendelea vizuri.
    Awali imeelezwa kwamba marehemu na majeruhi walifika kijijini hapo kutokea Ubaruku Mbarali kwa nia ya kwenda kwa mganga wa kienyeji kutafuta kizimba cha kilimo cha mpunga. Wakiwa bado wanasubiri huduma kwa mganga huyo ndipo kundi la watu likawavamia wakiwatuhumu kuwa ni wezi.
    Watuhumiwa watatu wamekamatwa kufuatia tukio hilo ambao ni 1. OBETH AMLIKE [43] Mwenyekiti wa kijiji cha Ngolela. 2. ITIKO KYOLO [64] mkazi wa Ngolela na 3. RUTH MGUNDA [26] mkazi wa Ngolela. Katika eneo la tukio kumekutwa shoka moja lenye damu, Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari na kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi. Upelelezi unaendelea.
    WITO:
    Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake wawafikishe watuhumiwa wanaowakamatwa kwa makosa mbalimbali katika mamlaka husika kwa hatua zaidi za kisheria. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu mapema kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
                                                     Imesainiwa na:
    [DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
    KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI