Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
ameteua timu mpya ya wataalamu saba kwa ajili ya kusimamia mradi wa
ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III), katika uwanja wa ndege
wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia agizo la Rais Dkt. John Magufuli
alilolitoa jana wakati alipofanya ziara ya kushtukiza uwanjani hapo
kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika mradi huo.
Timu hiyo inaongozwa na Eng. Julius Ndyamukama, Eng, Godson Ngomuo,
Eng. Humphrey Kanyenye, Eng. Abednego Lyanga, Eng. Mbila Mdemu na Eng.
Rehema Myeya.
“Naamini timu hii ina wataalamu mahiri, hivyo itasimamia ujenzi huu
kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha (value for
money”, amesema Mbarawa.
Aidha, ameitaka timu hiyo kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika mwezi Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Meneja wa mradi huo Eng. Julius Ndyamukama, ameahidi
kushirikiana na wenzake katika kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa
wakati.
Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amemsimamisha kazi Meneja wa
Fedha kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Simba Lugando
kwa kuidhinisha malipo ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Songwe mkoani
Mbeya kwa mkandarasi wa Kampuni ya DB Shapriea kiasi cha shilingi
Bilioni 3.3 ambapo ujenzi wake haukufanyika ipasavyo.

No comments:
Post a Comment