Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Serikali inafanya juhudi kubwa
katika kuhakikisha vijana wanapata ajira na wengine kujiajiri kwa
kufanya kazi mbalimbali zikiwemo za kujenga viwanda, kuanzisha miradi ya
kuwapatia wenzao ajira ikiwemo ya kilimo, mifugo, biashara ndogondogo
pamoja na ujasiriamali.
Sio kazi ya Serikali pekee bali
ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu na mafunzo
ya kutosha ili waweze kujiajiri au kuajiriwa na hatimaye kupunguza
utegemezi.
Hivyo Mashirika na Taasisi
mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinatakiwa kuhakikisha zinashirikiana
na Serikali katika kuwapatia vijana ajira na elimu ya kujitegemea kwani
ukuzaji wa ajira kwa vijana ndio kipaumbele kikubwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde anasema kuwa Serikali
ya awamu ya tano imejipanga kukuza ujuzi wa nguvu kazi kwa vijana ambao
utatolewa kupitia programu maalum ya mafunzo kazini kwa njia ya
Uanagenzi (Apprenticeship), mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu
(Internships) pamoja na urasimishaji wa ujuzi uliopatikana kwa mfumo
usio rasmi (Recognition of Prior Learning).
Mhe. Mavunde anakakaririwa
akisema kuwa, “Serikali yetu imetoa kipaumbele cha juu katika kujenga
ujuzi wa nguvu kazi, takribani vijana 15,000 watafaidika na programu
hiyo kwa mwaka huu wa fedha kwani tayari tumeanza kutekeleza kwa kuingia
mikataba na Makampuni ya kutoa mafunzo kwa vitendo katika maeneo ya
kazi”.
Kwa upande wa Mashirika, Shirika
lisilokuwa la Kiserikali la Plan International limejitolea kushirikiana
na Serikali katika kuwasaidia vijana nchini kujiwezesha kiuchumi kwa
kuratibu Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) ambao unawapa fursa
vijana wanaoishi katika mazingira magumu kuchangamkia fursa za elimu ya
ufundi zinazotolewa na Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA).
Mradi huo wa miaka mitatu
unafanyika katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Pwani na Dar es
Salaam, unatekelezwa kwa ushirikiano wa mashirika ya VSO, CCBRT, VETA,
UHIKI, CODERT pamoja na Serikali ya Tanzania huku ukiratibiwa na Shirika
la Plan International chini ya ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU).
Meneja wa Mradi huo, Bw. Simon
Ndembeka anasema kuwa mradi una lengo la kuwasaidia vijana wapatao 9100
ambapo asilimia 53 wakiwa wakike kupata elimu ya ufundi katika fani
mbalimbali ambapo nia na madhumuni ikiwa ni kuwajengea uwezo wa
kujiajiri au kuajiriwa na kuendesha maisha yao ili kupunguza kasi ya
umasikini nchini.
“Mradi huu umelenga vijana
wanaoishi katika mazingira magumu ambao wanatamani kujiendeleza kielimu
lakini hawana uwezo huo hivyo tunawasihi vijana mchangamkie fursa
iliyotolewa kupitia shirika letu ili muweze kuendeleza maisha yenu”,
alisema Ndembeka.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Plan
International-Tanzania, Bi. Gwynneth Wong amesema kuwa mradi umeokoa
vijana wengi kutoka katika mazingira hatarishi na kuwafanya wawe na
uwezo wa kujitegemea kwa kujishughulisha na biashara mbalimbali za
halali.
Ameongeza kuwa asilimia 65 ya
vijana 1225 waliohitimu mafunzo hayo wameajiriwa na wengine wamejiajiri
hivyo inaonyesha dhahiri kuwa miradi hii ya kuwainua vijana kiuchumi
inaleta mafanikio makubwa kwa vijana na taifa kiujumla.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi
wa YEE Kanda ya Mashariki, Adolf Jeremiah amesema kuwa mradi huo
hautoishia kuwapatia ujuzi tu bali utaendelea kuwawezesha kichumi ili
kuhakikisha vijana hao wanasimama imara na wanapata maendeleo kupitia
fani walizozisomea.
“Shirika la Plan International
tumeamua kusaidia vijana kwa hali na mali hivyo ni lazima kuhakikisha
wanayafikia malengo yao, kwa sasa tumewasiliana na VETA wafanye tathmini
ya vifaa vinavyotakiwa na vijana hao ili tuweze kuvinunua na kuwagawia
waendeleze fani zao zinazowasaidia katika maisha yao ya kila siku”,
alisema Jeremiah.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA –
Pwani, Joseph Deusdedit amesema kuwa kadri mradi unavyoendelea ndivyo
wavyozidi kutoa nafasi nyingi za vijana kupata elimu ya ufundi katika
chuo hicho pia wameendelea kuwatengea sehemu za kupata mafunzo zilizo
karibu na maeneo wanayoishi kwa ajili ya kuwawezesha kutambua kiurahisi
fursa zilizopo katika maeneo yanayowazunguka pia kuwapunguzia gharama za
usafiri.
“Nitajitahidi kushauriana na
wadau wengine kufanya elimu hii ya vijana wanaoishi kwenye mazingira
magumu kuwa endelevu hata kama mradi hautoendelea kwa sababu mradi huo
umeonyesha mafanikio na unalenga vijana wa aina zote wakiwemo walemavu,
waliosoma na wasiosoma hivyo kuondoa adha kubwa ya utegemezi katika
familia zao,” alisema Deusdedit.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha
Ufundi Stadi cha Future World, Robert Mkolla amesema kuwa ukosefu wa
ajira kwa vijana ambao ndio asilimia kubwa ya watanzania ni janga kubwa
kiuchumi na kiusalama kwani vitendo vingi viovu vinafanywa na vijana
wasio na kazi za kuwaingizia vipato hivyo shirika la Plan limeokoa
vijana wengi katika matatizo ya namna hiyo.
Mbali na kupewa mafunzo ya elimu
ya ufundi, Shirika la Uhamasishaji Hifadhi Kisarawe (UHIKI) linatoa
mafunzo ya kuweka na kukopa fedha kwa vijana waliohitimu mafunzo ya
ufundi chini ya mradi YEE ili kuwaelimisha jinsi ya kutunza fedha zao
Afisa Msimamizi wa Miradi ya
Kuweka na Kukopa – Kisarawe, Vuai Shame anasema kuwa kuna umuhimu wa
vijana kupata elimu juu ya utunzaji wa fedha pamoja na upatikanaji wa
mikopo ili waweze kuimarisha biashara zao na kuona faida inayopatikana
kutokana na biashara hizo.
“Kazi ya UHIKI ni kuwasimamia
vijana ili waweze kuunda vikundi vya kuweka na kukopa fedha
zitakazowasaidia kuendeleza biashara zao, mpaka sasa tumefanikiwa kuwa
na vikundi 27 vya vijana vilivyopo katika kata 4 za wilaya yetu lakini
bado tunaendelea kuwahamasisha vijana wengine kufanya hivyo kwani
vikundi vina faida”, alisema Shame.
Mradi huu unaendelea kuwasaidia
vijana wengi na umeonesha manufaa makubwa kwa jamii kiasi kwamba
Serikali inatambua mchango wao wa hali na mali.
Afisa Maendeleo ya Vijana wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Yahaya Mbogolume anasema kuwa mradi huo
umekuja wakati muafaka kwani umekuwa chachu ya maendeleo ya Halmashauri
hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni vijana ambao
walikuwa hawana cha kufanya lakini kupitia fursa hiyo vijana wameweza
kujiajiri.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii –
Kata ya Vingunguti, Pius Majura anasema kuwa, Sera ya Serikali ya Awamu
ya Tano ni kupunguza utegemezi kwa kuwasaidia vijana na wanawake kuweza
kusimama wenyewe kwa kufanya shughuli zao mbalimbali hivyo, mradi huo
umewasaidia vijana wa eneo hilo kuacha kufanya uhalifu na badala yake
wamejikita katika shughuli za halali ambazo zinawasaidia kupata kipato
cha kuwawezesha kuendesha maisha yao.
“Kabla ya mradi huu kuanza
vijana wengi walikuwa wakijihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya na
wasichana wengi walikua wakifanya biashara za kuuza miili yao, madanguro
yalikuwa mengi lakini baada ya vijana kupatiwa elimu na wengine kuweza
kujiajiri na kuajiriwa, uhalifu umepungua kwa asilimia kubwa”, alisema
Majura.
Kwa upande wake mmoja wa wahitimu
wa mafunzo ya mradi huo, George Geligoali anatoa rai kwa vijana wenzie
kuacha kudharau fursa zinazotolewa na makampuni mbalimbali na badala
yake wazichangamkie kwa kuwa fursa hizo ni kwa ajili ya maendeleo yao na
Taifa kiujumla.
Mhitimu mwingine Rajabu Kilanga
anasema kuwa mradi huo umemuwezesha kufahamu jinsi ya kuhifadhi fedha
kwa ajili ya maisha ya baadaye pia umemnufaisha yeye pamoja na familia
yake kwani kupitia fani ya umeme aliyoisomea ameweza kupata tenda ndogo
ndogo ambazo zinamsaidia kuyaendesha maisha yake.
“Pamoja na faida nyingi
nilizozipata kupitia mradi huu lakini ukosefu wa ajira za kudumu ni moja
ya changamoto ambazo zinatukabili vijana tuliohitimu mafunzo haya
hivyo, tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia ajira ili na sisi tuweze
kutimiza malengo yetu na kuchangia katika kulijenga Taifa letu”, alisema
Kilanga.
Mradi wa Uwezeshaji Vijana
Kiuchumi (YEE) -Tanzania, pia unashughulika na kuwasaidia wanafunzi
wenye mahitaji maalumu kupata Elimu ya ufundi kwani jamii bado
haijatambua umuhimu wa kuwapatia elimu watu wenye ulemavu
No comments:
Post a Comment