Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na
Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali
imejipanga kusaidia vijana kutambua na kuchangamkia fursa mbalimbali za
ajira zilizopo nchini ili kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na kutimiza
adhma ya kuleta maendeleo hususani kwa vijana.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo jana wakati akijibu
hoja ya Mbunge wa Kinondoni Mhe. Maulid Mtulia iliyohoji juu ya jitihada
za Serikali katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wakati wa
Mkutano wa Tano wa Bunge unaoendelea Mkoani Dodoma.
Katika Mkutano huo Mhe. Waziri alisisitiza kuwa Serikali
ina mipango na mikakati madhubuti inayokusudiwa yakusaidia vijana wa
Kitanzania ili kujiletea maendeleo yao wenyewe na kuondokana na umasikini.
“Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuweka
mikakati ikiwemo uwanzishwaji wa programu mbalimbali zitakazo saidia kutatua
changamoto ya ajira kwa vijana kwa kuangalia matokeo ya tafiti mbalimbali
ambazo zimepelekea kuwa na programu zinazolenga kukabili tatizo la ukosefu wa
ajira kwa vijana” Alisema Waziri
Alisisitiza kuwa programu hizo ni pamoja na; kurasmisha
ujuzi usio rasmi kuwa rasmi, mfumo wa mafunzo kwa vitendo, mfumo wa uanangezi
pamoja na kukuza mafunzo kwa watanzania kulingana na soko lililopo kwa sasa.
Pamoja na juhudi hizo zinazotarajiwa kuzaa matunda bado
Waziri aliwatoa hofu wananchi wote kwa kuwepo kwa fursa hizo za ajira zitakazo
jali hali za watu pasipo kuangalia makabila yao, rangi wala dini.
“Katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana hatuta angalia
kabila, rangi wala dini ya mtu bali kutakuwa na
haki na usawa”.Alisisitiza Waziri
Aliongezea kuwa, Serikali pia inajitihada za
kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali na urasimishaji wa sekta isiyo rasmi
ili kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira.
“Serikali itatumia sekta zenye uwezo wa kutoa
ajira kwa wingi ikiwemo zile za Kilimo, majenzi, Mawasiliano na Utalii ili
kuzitumia kuweka mazingira mazuri kwa vijana kupata fursa za ajira”.
Mhe. Mhagama alisisitizia bungeni kuwa kutokana
na tafiti mbalimbali zilizofanyika zitatumika kama chachu ya kuangalia maeneo
yanayohitaji kusaidia kwa haraka na kupunguza changamoto hiyo kwa vijana.
“Kwa kuangalia tafiti ya Hali ya Ajira Nchini
ya mwaka 2014 imeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua kutoka
asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3 mwaka 2014 na ukosefu wa ajira
kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka
2014”,alisema.
No comments:
Post a Comment