Serikali imesema katika kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni,
Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza
usimamizi katika maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ambapo taarifa
za kila muamala wa fedha za kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Igunga Mhe.
Dalaly Peter Kafumu aliyetaka kupewa ufafanuzi juu ya Kwanini Serikali
isidhibiti matumizi holela ya dola nchini ili kupunguza utakasishaji wa
fedha na kuimarisha ukuaji wa uchumi kama zinavyofanywa nchi nyingi
duniani.
Dkt Kijaji alifafanua kuwa hatua zimechukuliwa kuhakikisha kuwa
miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na mabenki ni ile inayohusu
shughuli za kiuchumi tu ili kulinda thamani ya shilingi.
Vilevile, tamko na mwongozo uliotolewa na Serikali mwaka 2007,
ulieleza kuwa bidhaa na huduma zinazowalenga watalii au wateja wasio
wakazi wa Tanzania, bei zake zinaweza kunukuliwa kwa sarafu mbili, yaani
shilingi ya kitanzania na sarafu ya kigeni na malipo kufanyika kwa
sarafu ambayo mlipaji atakuwa nayo. Pia, mkazi yeyote wa Tanzania
asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za
kigeni.
“Msingi wa kuruhusu soko huru la fedha za kigeni hapa nchini ni hatua
ya makusudi ambayo ilichukuliwa na Serikali ili kuiwezesha nchi
kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha za kigeni ilikuwa dola za
Kimarekani milioni 4,093.7 wakati amana za fedha za kigeni za wakazi wa
Tanzania zilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,933.1 na rasilimali za
fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni
1,021.1” alisema Kijaji.
Dkt Kijaji ameeleza kuwa Tanzania ina urari wa biashara ya nje ambao
umetokana na sera huru za kigeni, ambazo zimechangia kuimarisha uchumi
kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa
katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ulikua ni asilimia 7, ikiwa ni
wastani wa juu sana ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.
“Mfano, wastani wa ukuaji wa uchumi wa nchi za kusini mwa jangwa la
Sahara ni asilimia 5.4 katika kipindi hicho wakati ule wa nchi
zinazoibukia kiuchumi ulikua ni asilimia 5.8” alisisitiza Dkt. Kijaji
Alisema kuwa njia zinazotumika kutakatisha fedha ni pamoja na
kuziingiza haramu kwenye taasisi za fedha na kuziwekeza katika
rasilimali halali kama ardhi na nyumba. Baadhi ya mambo yanayowapatia
wahalifu fedha haramu ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya, rushwa,
ujangili, ujambazi, ukwepaji kodi n.k. Aidha fedha zinazotokatana na
shughuli za kihalifu zinaweza kuwa shilingi za Kitanzania, dola za
Kimarekani au fedha nyingine yoyote ile.
Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango amesema ziko kanuni ambazo
zinafuatwa na vyombo vya fedha ili kuzuia utakatishaji wa fedha zote
zilizopatikana kutoka vyanzo haramu na sio dola pekee huku akibainisha
kuwa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la usimamizi wa taasisi za fedha,
kufuatilia mabenki ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinafuatwa.

No comments:
Post a Comment