Akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo 16 Februari 2017, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu amebainisha kuwa kila msafiri atatakiwa kupata chanjo halali na kupewa cheti maalumu cha chanjo ya Homa ya Manjano yaani ‘International Certificate of Vaccination’ kama utambulisho kwamba amepata chanjo ya Homa ya Manjano.
“Wizara imefanya maboresho ya vyeti vya chanjo ya Homa ya Manjano ambavyo nilivizindua tarehe 24/11/2016. Lengo likiwa ni kudhibiti utolewaji holela wa vyeti hivi. Vyeti hivi vipya vilianza kutolewa kuanzia tarehe 1 Agoslinaendelea kutolewa katika vituo vya Afya vya Serikali vilivyo idhinishwa hadi sasa” ameeleza Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu pia ameongeza kuwa, Wananchi wote wenye vyeti vya chanjo ya Homa ya Manjano vya zamani ambao walipatiwa chanjo na kupewa vyeti halali kuwa, wawasilishe vyeti hivyo na hati ya kusafiri kwenye kituo cha Afya alichopatiwa cheti ambako kumbukumbu za chanjo zipo ili aweze kupatiwa cheti kipya. Gti, 2016 zoezi likienda kwa gharama ya Tsh. 5000 na kwa raia wa Kigeni ni Dola 10 pekee.
Chanjo hiyo hutolewa kwa wasafiri wanakwenda kwenye nchi 30 za Bara la Afrika ambazo ni Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameron, Afrika ya Kati, Chad, Congo, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Equatorial Guinea, Ethiopia, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Ginea Bissau, Kenya, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Sudan ya Kusini, Sudan, Togo, Uganda.
Pia kwa nchi 13 kutoka Bara la Amerika ya Kusini ambazo ni Argentina, Bolivia, Brazil, Colombia, Ecuador, French Guiana, Guyana, Panama, Paraguay, Peru, Suriname, Trinidad, Venezuela kama zilivyoainishwa na WHO kuwa na hatari ya maambukizi ya ugonjwa wa Homa ya Manjano Wasafiri wanaokwenda nchi hizi wahakikishe wanachanja chanjo ya Homa ya Manjano siku 10 kabla ya kusafiri na kisha kupewa cheti cha kuthibitisha kupata chanjo hiyo.
Mkutano huo ukiendelea
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy Mwalimu amekitupia lawama kituo
cha Mnazi Mmoja kwa hatua yake ya kutoa vyeti vya Chanjo bila kuchanjwa.“Ni wajibu wa kila msafiri nchini kuepuka kupokea au kununua vyeti vya chanjo ya manjano bila kupata chanjo kwani kufanya hivyo sio tu ni kosa la jinai bali pia kunahatarisha maisha ya msafiri na ya watu wengine. Aidha, ninawaomba wananchi kutoa taarifa kwenye ofisi yoyote ya Serikali iliyo karibu au vyombo vya dola endapo watabaini Afisa au mtu anatoa cheti cha njano bila chanjo hiyo kutolewa.
Kitendo hiki ni kinyume na Sheria ya Afya Jamii ya Mwaka, 2009. Hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote anayetengeneza, kuuza au kununua vyeti visivyo halali vya chanjo” alieleza Ummy.
Ameongezea kuwa, Zoezi hilo la kubadilisha vyeti vya zamani vya chanjo ya manjano limeanza tangu tarehe 09 Januari, 2017 na litadumu hadi tarehe 31 Machi, 2017. Kuanzia tarehe 01 Aprili, 2017 vyeti vya zamani vya chanjo havitatambulika tena hivyo wananchi wote wenye vyeti halali vya zamani wawasilishe vyeti hivyo kwenye vituo vya Afya walikopatiwa Chanjo ya Homa ya Manjano ili vibadilishwe.
Vituo hivyo ni pamoja na Viwanja vya Ndege wa Kimaitaifa wa Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Pia katika bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga, Bandari ya Mwanza na Bandari ya Kigoma.
Katika mipaka ya nchi kavu ni pamoja na Horohoro, Namanga, Holili, Tarakea, Sirari, Isaka, Mutukula, Mtambaswala, Kasumulu na Tunduma. Huku kwa Jiji la Dar es Salaam, ni pamoja na kituo cha Mnazi Mmoja.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) mapema leo wakati wa kuzungumzia suala hilo la vyeti vipya vya homa ya Manjano. Anayefuatia ni Mkurugenzi wa Uhakiki na Ubora wa Huduma za Afya Dk. Mohammed Mohammed
No comments:
Post a Comment