Na Jumia Travel Tanzania
Kama sio
mwenyeji wa jiji la Dar es Salaam basi ni vema ukauliza kwanza kabla ya
kuhamia sehemu na kuanza kuishi. Usipofanya hivyo kwenye kipindi cha
mvua kama hiki usishangae unaamka ukiwa umezungukwa na maji kama sio
kuelea kabisa.
Kuwa na
vipindi virefu vya jua na joto kali haimaanishi kuwa maeneo yote ya Dar
es Salaam hubakia hivyo mwaka mzima. Jumia Travel imekusogezea maeneo
haya 5 ambayo miaka nenda rudi lazima yakumbwe na mafuriko.
Jangwani
Umaarufu
wa Jangwani ni kwamba mvua ikinyesha tu, bila hata ya kutazama taarifa
ya habari utajua ni lazima mafuriko yamelikumba eneo hilo. Na hii yote
ni kutokana na jiografia ya eneo hili kupakana na mto Msimbazi ambao
hupokea maji kutoka mito mbalimbali jijini Dar es Salaam kuelekea bahari
ya Hindi ambayo ipo mita chache tu. Kwa muda mrefu wakazi wa eneo hili
wamekuwa wakiambiwa na serikali kuhama lakini wamekuwa ni wakaidi.
Sababu kubwa inayowafanya wakazi wengi kuling’ang’ania eneo hili ni kwa
sababu lipo karibu na katikati ya jiji pamoja na huduma lukuki za
kijamii kama vile usafiri. Wakazi wengi wanaoishi eneo hili hutembea kwa
miguu kufika maeneo ya kazi.
Tandale
Kutokana
na msongamano mkubwa wa makazi ya watu imekuwa ni vigumu sana kwa maji
kupita kwenye njia yake. Kwa kiasi kikubwa eneo hili lipo kwenye mkondo
wa maji na ndio sababu inayopelekea kukumbwa kwa urahisi na mafuriko.
Urahisi wa upatikanaji na unafuu wa vyumba vya kupanga katika eneo hili
usikudanganye na kujikuta ukataka kuishi. Siku zote nafuu ni gharama
kama walivyosema wahenga. Ni kweli maisha ya Tandale ni ya chini sana
lakini nakuhakikishia gharama utakazokuja kuingia kipindi cha mafuriko
utajuta kulifahamu hilo eneo.
Buguruni kwa Mnyamani
Eneo la
Buguruni lipo kwenye Wilaya ya Ilala ambayo ni maarufu kwa shughuli
mbalimbali za kibiashara kama vile masoko ya Karume, Buguruni na
Kariakoo. Ikiwa imezungukwa na biashara mbalimbali pamoja na huduma
lukuki za kijamii, sio Buguruni yote ni mahali salama kwa makazi ya
watu. Ikifika kipindi cha mafuriko Buguruni nayo huingia kwenye anga za
habari za waathirika hususani eneo la kwa Mnyamani. Eneo hili kama
maeneo mengine yanayokumbwa na mafuriko, wakazi wamejenga kwenye vyanzo
vya maji na kuviziba kabisa.
Kuna
athari kubwa sana za kuzuia njia ya maji kwani yakifurika huwa
hayachagui mahali pa kupita. Hivyo basi usije ukarogwa ukakubali kwenda
kuishi eneo hili hata kama chumba ni bure.
Msasani Bonde la Mpunga
Kutokana
na ukaribu wake na katikati ya jiji, eneo hili limevutia uwekezaji
mkubwa wa majengo kadhaa ya kibiashara kama vile hoteli, maduka makubwa
ya bidhaa, migahawa, ofisi, kumbi za filamu na mikutano, na kadhalika.
Kwa asilimia kubwa wakazi wa eneo hili ni mchanganyiko wa maisha duni na
wa hali ya kati.
Eneo hili
nalo ni sehemu ambayo miaka yote hukumbwa na mafuriko na sababu kubwa
ni kwamba eneo hili lina asili ya majimaji. Sababu pekee ambazo
zinawafanya watu kung’ang’ania eneo hili licha ya mafuriko ni
upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii, uwepo wa vitega uchumi
vingi hivyo kutoa fursa za ajira lakini pia ni takribani kilometa 6
mpaka kufika katikati ya jiji. Hivyo endapo utakwenda kuishi eneo hili
tegemea kwamba kila ifikapo kipindi cha mvua basi ujue mafuriko ni
lazima.
Eneo
kubwa la Kigogo limepakana na mto Kigogo ambao hupokea maji kutoka
mifereji mbalimbali na kisha kuungana na mto Msimbazi ambao humwaga maji
yake katika bahari ya Hindi. Kutokana na wakazi wengi kujenga pembezoni
mwa mto huu, ni jambo la kawaida ikifika kipindi cha mvua kukumbwa na
mafuriko.
Mvua
zikiwa kubwa sana mto hutapika kwenye kingo zake na kusambaa eneo la
karibu yake ambalo kwa kiasi kikubwa limevamiwa na makazi ya watu.
Wakazi wa eneo hili ni mchanganyiko wa maisha ya chini na ya kati mbali
na hapo pia ni karibu kufika katikati ya jiji ukiwa unaishi Kigogo.
Kama
utakuwa umegundua kitu ni kwamba wakazi wengi katika maeneo yaliyotajwa
hapo juu wana sababu zinazofanana. Wengi wameng’ang’ania maeneo hayo
kutokana na upatikanaji wa huduma za kijamii, unafuu wa maisha pamoja na
ukaribu wa katikati ya jiji ambapo ndipo hufanyia shughuli zao. Lakini
hizo hazitoshi kuwa sababu za kuhatarisha maisha yako, Jumia Travel
inakushauri kwamba siku zote huduma za kijamii huwafuata watu na sio
kinyume chake





No comments:
Post a Comment