Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Juma (wa pili kushoto) akiwasili katika ukumbi wa
AICC jijini Arusha kuhudhuria Mafunzo ya Majaji yaliyoanza leo jijini
humo.Kushoto kwake ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.
Ferdinand Wambali. Kushoto kwa Jaji Wambali ni Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania Mhe. Katarina Revokati na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa
Utawala wa Mahakama Bibi Wanyenda Kutta.
……………………………………………………………….
Na Lydia Churi-MAHAKAMA, ARUSHA
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Mheshimiwa Ferdinand Wambali amewataka Majaji wa Mahakama Kuu
nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia Maadili, kuwa waaaminifu na
kushirikiana katika kuwahudumia wananchi ili kesi zimalizike kwa haraka
katika Mahakama mbalimbali.
Akifungua Mafunzo ya siku tano ya
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tazania kuhusu Uongozi katika shughuli za
Mahakama leo jijini Arusha, Jaji Kiongozi amesema lengo la Mafunzo hayo
ni kujadiliana kwa kina nini kifanyike ili kesi zimalizike mapema
kwenye mahakama mbalimbali nchini.
Jaji Wambali alisema katika
mkutano huo, Majaji watapata nafasi ya kujifunza Mpango Mkakati wa Miaka
Mitano wa Mahakama ya Tanzania wenye nguzo tatu ambazo ni pamoja na
masuala ya Utawala, Upatikanaji wa haki kwa wakati na imani ya wananchi
kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama.
Katika Mafunzo hayo pia Majaji
watajadiliana ni nini kilifanyika mwaka jana katika umalizwaji wa
mashauri, changamoto zilizojitokeza na nini kifanyike ili kutatua
changamoto zinazojitokeza katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati akizungumza na Waandishi wa habari
kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo alisema yamegawanyika katika makundi
matatu ambapo kundi la kwanza ni la Majaji wa Mahakama ya Rufani, kundi
la pili ni la Majaji Wafawidhi wa Kanda 14 za Mahakama Kuu ya
Tanzania na kundi la Tatu ni la Majaji wengine wote.
Alisema Majai wa Mahakama ya
Rufani watapatiwa Mafunzo kuhusu namna ya kutoa maamuzi ya Mahakama
katika usikilizwaji wa kesi ngazi ya Rufaa, ambapo Majaji Wafawidhi
watapewa mafunzo kuhusu Usimamizi wa uendeshaji wa kesi wakati Majaji
wengine watapatiwa mafunzo kuhusu uongozi na usimamizi wa kuleta
mabadiliko.
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na
Benki ya Dunia ni Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa
Mahakama ya Tanzania na yanalenga katika kuboresha utendaji kazi na
kuleta mabadiliko ndani ya Mahakama
No comments:
Post a Comment