Tanzania na Uganda zimetakiwa
kushirikiana kwa pamoja kutumia rasilimali walizonazo kutatua changamoto
zinazowakabili wananchi wa pande zote mbili.
Kauli hiyo imetolewa leo kwa
pamoja jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, Balozi Patrick Mugoya walipokuwa
wanafungua Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati
ya nchi hizo mbili.
Walieleza kuwa kikao hicho ni cha
kwanza kufanyika tokea makubaliano yaliposainiwa mwaka 2007 na
kinafanyika kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati
wa ziara ya Rais Yoweri Museveni nchini mwezi Februari 2017.
“Kikao hiki ni fursa kwa wataalamu
wetu kujadili na kubuni mfumo bora na endelevu wa Ushirikiano
utakaoleta tija kwa pande zote mbili katika kila eneo iwe miuondombinu,
biashara, viwanda, uwekezaji, usafiri wa anga na majini, kilimo, elimu,
afya, mazingira, utalii, nishati na ufugaji.
Balozi Mwinyi alieleza kuwa licha
ya nchi hizo mbili kuwa na mahusiano mazuri tokea miaka ya 60 lakini
kiwango cha biashara kati yao ni kidogo mno hivyo aliwashauri wajumbe wa
JPC kubuni mikakati itakayonyanyua kiwango cha biashara.
Kwa upande wake, Balozi Mugoya
aliwambia wajumbe wa kikao hicho kuwa Tanzania na Uganda sio tu ni nchi
majirani, bali ni nchi zenye urafiki mkubwa, hivyo alihimiza urafiki huo
utumike kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa pande zote.
” Tuna changamoto za ukame, uhaba wa maji na malisho kwa wafugaji na
wakulima wanaoishi katika mipaka yetu. Hivyo alisisitiza umuhimu wa
kikao hicho kutoa mapendekezo ya namna ya kushirikiana kwa kutumia
rasilimali zilizopo mipakani na nyinginezo kukabiliana nazo”.
Kikao hicho cha JPC kitafungwa
rasmi siku ya Jumatano na Mawaziri wa Mambo ya Nje ambapo kabla ya
kufungwa kutashuhudiwa uwekaji saini wa makubaliano mbalimbali kati ya
Tanzania na Uganda. Makubaliano hayo ni pamoja na Ushirikiano katika
kuboresha bandari, usafiri wa majini na huduma ya usafiri wa reli;
kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la
Kikagati/Murongo; Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na
lile la Uganda katika masuala ya usalama, Ushirikiano kati ya Wizara ya
Elimu, Sayansi naTeknolojia na Wizara ya Elimu ya Uganda, Ushirikiano
kati ya Shirika la Utangazaji la Tanzania na la Uganda na Ushirikiano
katika huduma za usafiri wa Anga.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 03 Aprili, 201
No comments:
Post a Comment