Mkurugenzi
wa Miradi kutoka shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare
Initiative (AGPAHI) Dk. Safila Telatela akizungumza wakati wa kufungua
Ariel Camp (Kambi ya Ariel) ya siku tano kuanzia June 19,2017 – June
23,2017 iliyokutanisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya
Shinyanga,Mwanza na Geita jijini Mwanza.Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mratibu
wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza Dk. Pius Maselle akifungua kambi ya watoto
na vijana ‘Ariel Camp’ katika hotel ya Lesa Garden jijini Mwanza.Wa
kwanza kushoto ni Mratibu wa Miradi AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Gastor
Njau akifuatiwa na Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Geita Dk. Joseph Odero.
Wa kwanza kulia ni Mratibu wa Miradi AGPAHI mkoa wa Mwanza, Olympia
Laswai akifuatiwa na Mkurugenzi wa Miradi AGPAHI, Dk. Safila Telatela.
*****
Jumla ya watoto 8,615 kutoka mikoa ya
Tanga, Mara, Mwanza,Geita, Simiyu na Shinyanga wamepatiwa huduma za
Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ikiwemo kupatiwa dawa za kupunguza makali ya
VVU (ARVs) katika kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi mwezi Machi 2017.
Huduma hizo zimetolewa na shirika la
Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI)
linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi
kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na
Watoto.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa
Miradi kutoka AGPAHI,Dk. Safila Telatela wakati wa kufungua Kambi ya
Ariel ‘Ariel Camp’ ya siku tano inayokutanisha watoto na vijana wenye
umri kuanzia miaka 10 mpaka 17 kutoka mikoa ya Shinyanga,Geita na Mwanza
inayofanyika katika Hotel ya Lesa Garden jijini Mwanza.
Dk. Telatela alisema watoto hao ni sawa
na asilimia 5 kutoka jumla ya watu 189,806 waliopatiwa huduma na shirika
hilo katika kipindi hicho na shirika linaendelea na kazi ya kutoa
matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 katika mikoa hiyo sita.
Alisema pia wanafanya kazi ya kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto katika vituo 631.
Aidha Dk. Telatela alisema wamefanikiwa
kuunda vikundi zaidi ya 65 vya watoto na vijana katika mikoa ya
Shinyanga na Simiyu ambapo takribani watoto 2640 wamenufaika na vikundi
hivyo.
“Kuanzia mwezi Oktoba 2016, shirika
letu limeongeza wigo wa kutoa huduma kutoka mikoa miwili ya Shinyanga na
Simiyu na sasa imekuwa sita na tunafanya kazi ya kutoa matunzo na tiba
za VVU katika vituo 553 kwenye mikoa hii sita”,alieleza Dk. Telatela.
“Shirika letu limekuwa likiandaa
kambi kwa ajili ya watoto na vijana kwa lengo la kuwakutanisha ili
kujifunza mambo mbalimbali kuhusu afya, stadi za maisha, kupata ushauri
wa kisaikolojia kutokana na changamoto wanazokutana nazo na pia huduma
za kitabibu kutoka kwa daktari wa watoto katika kipindi chote cha kambi
na kuwafanya kuwa mabalozi wa huduma za watoto katika jamii zao”,aliongeza.
Naye Mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa
kambi hiyo, Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Pius Maselle alitoa
rai kwa mikoa mipya ya AGPAHI (Geita,Tanga,Mara na Mwanza) kufanya
jitihada za ziada katika uundaji wa vikundi vya watoto na vijana ili
idadi ya watoto watakaonufaika na huduma za kisaikolojia iwe kubwa.
Aidha Dk. Maselle alitoa shukrani kwa
shirika la AGPAHI kwa jitihada mbalimbali linazofanya katika mapambano
dhidi ya VVU na Ukimwi nchini kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia
shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa
kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na
Shirika la Development Aid From People to People (ADPP – Mozambique).
HII
HAPA HOTUBA FUPI YA UFUNGUZI WA KAMBI YA WATOTO NA VIJANA (ARIEL CAMP)
2017 ILIYOTOLEWA NA MKURUGENZI WA MIRADI AGPAHI,DR. SAFILA TELATELA
Ndugu,
· Mgeni rasmi – Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Mwanza,
· Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa wa Geita,
· Wafanyakazi wa AGPAHI,
· Watumishi wa afya walioambatana na watoto (walezi wa watoto)
· Watoto wa Kambi ya Ariel,
· Waandishi wa Habari,
· Mabibi na Mabwana.
Habarini za asubuhi!
Awali
ya yoye, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wageni wote katika
hafla hii fupi ya ufunguzi wa kambi yetu ya nane (8) tangu kuanzishwa
kwa shirika la AGPAHI mwaka 2011. Pia napenda kutoa shukrani kwenu wote kwa kujumuika na sisi hapa siku hii ya leo, Asanteni sana!
Nichukue
fursa hii kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika la AGPAHI kuwashukuru
wafanyakazi wenzangu wa AGPAHI na walezi wa watoto kutoka Geita,
Shinyanga na Mwanza kwa kushiriki katika kuandaa kambi hii tangu hatua
za awali za kuwachagua watoto na vijana huko vituoni kwao, kuwasafirisha
na kuwafikisha hapa Lesa Garden – Mwanza. Hongereni sana na Mungu
awabariki!
Ndugu
mgeni rasmi, napenda kutoa shukrani kwa Watu wa Marekani kupitia
shirika lao la CDC ambao ndio wahisani wa kambi hii. Hata hivyo tuna
wafadhili wetu wengine wa miradi kama vile Children Investment Fund
Foundation (CIFF) and Development aid from People to People (ADPP –
Mozambique). Tunawashukuru sana.
Ndugu mgeni rasmi,Shirika la AGPAHI ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeshwa na watanzania na watanzania wenyewe ndio sisi hapa.
Shirika
letu lilianzishwa mwaka 2011 kutokana na dira ya serikali ya Tanzania
na ile ya wafadhili yaani serikali ya Marekani kutaka wazawa (serikali
pamoja na mashirika yasiyo ya serikali) kuendesha miradi mbalimbali
inayoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI na masuala ya afya ya mama na
mtoto ili kuwa na miradi endelevu.
Kuanzia
mwezi Oktoba 2016, shirika letu limeongeza wigo wa kutoa huduma kutoka
mikoa 2 hadi sita ambayo ni Tanga, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na
Shinyanga. Huduma zitolewazo ni pamoja na tiba na matunzo kwa watu wenye
VVU, kuzuia maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto, uchunguzi
wa awali na tiba ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa huduma
shirikishi za kifua kikuu na UKIMWI sehemu za migodini.
Takwimu
Ø AGPAHI
inafanya kazi ya kutoa matunzo na tiba za VVU katika vituo 553 kwenye
mikoa sita (Tanga, Mara, Mwanza,Geita, Simiyu na Shinyanga).
Ø Huduma ya kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto katika vituo 631.
Ø Kutoa huduma ya uchukuaji wa sampuli ya damu kavu kwa watoto katika vituo 631.
Ø Huduma
shirikishi za kifua kikuu na Ukimwi katika maeneo manne (5) ya migodi
(Mererani, Iyenze, Mwime, Kalole, Kakola na Mwazimba).
Ø Hadi
mwezi Machi 2017, jumla ya watu waliowahi kupata huduma za VVU/Ukimwi
ikiwemo kupata dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) ni 189,806 kati yao
watoto walikuwa 8615, hii sawa ni asilimia 5%.
Ø AGPAHI
pia inatoa huduma mseto za uzazi wa mpango katika vituo vya ushauri
nasaha na upimaji wa hiari na tiba na matunzo vinavyowezeshwa na AGPAHI.
Kwa
kutambua umuhimu wa watoto na vijana, Shirika la AGPAHI lilianzisha
huduma za kisaikolojia kwa kupitia vikundi vya watoto tangu mwaka 2011
pindi lilipoanzishwa (ambapo Shirika lilikuwa linafanya kazi katika
mikoa ya Shinyanga na Simiyu). Huduma hizo zilihusisha uundwaji wa
vikundi vya watoto na vijana katika vituo vya kutolea huduma za afya
(yaani CTC).
Kwa
sababu ya umuhimu wa vikundi hivi, AGPAHI imeshaanza juhudi za makusudi
za kuanzisha vikundi kwenye mikoa minne (4) ambayo tumeanza kufanya
kazi tangu Oktoba 2016 (Mwanza, Mara, Geita na Tanga). Azma yetu ni
kuhakikisha tunawaunganisha watoto na vijana wengi kwenye huduma za
kisaikolojia kwa kupitia vikundi.
Kutokana
na uundwaji wa vikundi vya huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana,
AGPAHI ilifanya juhudi za kuanzisha kambi za watoto ambazo hufanyika
mara moja au mbili kwa mwaka. Kambi hii tunayoizindua leo ni kambi ya
nane (8) kufanyika chini ya uratibu wa shirika la AGPAHI (kwa mwaka huu
hii ni kambi ya pili kufanyika). Kambi nyingine za awali zimeshanyika
katika mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Mwanza. Utaratibu huu wa
kuwapeleka watoto na vijana kwenye kambi zilizopo maeneo tofauti ni
mzuri kwani unasaidia kuwafundisha mambo mengi kuhusu nchi, historia na
tamaduni bila kusahau masomo wanayopata wakiwa kambini.
Ndugu mgeni rasmi,
Kambi hii inahusisha watoto na vijana kutoka katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Mwanza
yenye jumla watoto 50 na watumishi wa afya (walezi wao) 11. Watoto
pamoja na watumishi wa afya wametoka katika vituo mbalimbali kama
walivyotambulishwa awali. Wana umri kati ya miaka 10 -17.
Washiriki
wa kambi wakiwa hapa kambini hufundishwa kuhusu afya na makuzi, lishe,
stadi za maisha, elimu sahihi kuhusu VVU na Ukimwi, ufuasi mzuri wa dawa
pamoja na unyanyapaa na unaguzi.
Pia
hupata ushauri wa kisaikolojia kutokana na changamoto wanazokutana nazo
na pia huduma za kitabibu kutoka kwa daktari wa watoto katika kipindi
chote cha kambi.
Vilevile,
naomba kuchukua fursa hii, kuwasihi watoto na vijana kuzingatia elimu
na kanuni za afya kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya na endeleeni
kuwa wanachama wazuri katika vikundi vyenu na muwe mabalozi wa
kuwahamasisha watoto na vijana wenzenu kujiunga na vikundi.
Mwisho
ningependa kuwashukuru watumishi wa afya mliokuja na watoto kutoka
Geita, Shinyanga na Mwanza. Nawasihi muendelee kuwajenga na kuwasimamia
watoto ili wawe mabalozi wazuri kwa wengine, ili baadae tujivunie
ushiriki wao katika kambi ya Ariel 2017


No comments:
Post a Comment