Na
Rhoda James - Dodoma
Imeelezwa kuwa
Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) itazalisha Megawati 200-600
kutokana na Jotoardhi ifikapo 2025.
Kauli hiyo imetolewa
jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani katika
Semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini.
Dkt. Kalemani
ameielezea Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini kuwa TGDC ina jukumu
la kuendeleza nishati ya Jotoardhi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania ili kukuza
uchumi na kuongeza ajira.
Aliongeza kuwa, Tanzania
ina reserve ya Jotoardhi
inayokadiliwa kuzidi Megawati 5000 na inapatikana maeneo mbalimbali nchini ikiwa
ni pamoja na Mbeya, Songwe, Rukwa, Dodoma, Singida, Shinyanga, Morogoro, Pwani,
Mara, Kagera na Arusha.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi
Kato Kabaka ameieleza Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuwa, Kampuni ya
TGDC ina majukumu mengi likiwemo jukumu la kuendelea kuhimiza matumizi mengine
ya nishati ya Jotoardhi (direct heat use).
Aliongeza kuwa TGDC
itaanza kuzalisha megawati 30 ifikapo 2018 kutoka Mradi wa Ngozi ambapo utafiti
umefanyika kwa kiasi kikubwa.
Mhandisi Kabaka ameelezea
upatikanaji wa jotoardhi ambao unatokana na mchakato wa kinyukilia ndani ya
tufe la dunia, ambalo ni endelevu na mchakato huu hutokea kwenye nyufa zilizopo
kwenye gamba la dunia.
Aidha, ameeleza kuwa
tofauti na upatikanaji wa nishati ya umeme, jotoardhi inajumuisha vitu vingi
ikiwa ni pamoja na gesi ya Carbon oxide, sulphur na madini mbalimbali ambayo
hutumika viwandani na manyumbani.
“Jotoardhi hutumika
katika ukaushaji mazao ya kilimo, uzalishaji wa mbogamboga, ufugaji wa samaki,
utalii wa kibiashara, mabwawa ya kuogelea na usambazaji wa Joto kwenye Nyuma,”
Alisema Mhadisi Kabaka.
Pia, Mhandisi Kabaka
alisema kuwa uzalishaji wa Jotoardhi ni rafiki kwa mazingira ukilinganisha na
vyanzo vingine vya nishati ya umeme.
Aliongeza kuwa ipo
haja ya Kampuni ya TGDC kuwa na Sheria ambayo itasaidia katika Uendelezaji wa
Jotoardhi na kuagiza Wizara, sasa kuhakikisha kuwa TGDC hailipia leseni ya utafiti
ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa nishati hiyo.
Jotoardhi inazalishwa
katika nchi zaidi ya 26 duniani na zaidi ya Gigawati 12.6 zilipatika mwaka
2015, na zaidi ya nchi 90 zina maeneo yenye rasilimali ya jotoardhi.
No comments:
Post a Comment