Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akipokea maelezo kutoka kwa Mkuregenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara
(MTUWASA), Inj. Mashaka Sitta alipotembelea chanzo cha maji cha
Mtawanya, mkoani Mtwara pamoja na Inj. Najib Asumbwile kutoka Wizara ya
Maji na Umwagiliaji.
Sehemu ya Mtambo wa Kusafishia Maji, mkoani Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akikagua sehemu ya majengo mapya ya
Ofisi za Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini ambayo ujenzi wake
unaendelea, akiwa na Afisa Bonde, Msiru Msengi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza kwenye ofisi ya Katibu
Tawala Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mara baada ya kupokea taarifa ya
utekelezaji wa miradi ya maji mkoa wa Mtwara.
……………………….
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi
wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA) ifanye bidii na kuhakikisha Mtwara
inapata maji kwa asilimia 100, ikizingatiwa ni mji ulio na viwanda
vikubwa, ili kuunga mkono Sera ya Viwanda inayotekelezwa na Serikali.
Prof. Mkumbo alisema hayo
katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya mkoani Mtwara, alipokuwa
akitembelea mamlaka hiyo kwa nia ya kujua utendaji kazi wake na mipango
ya utekelezaji wa miradi yake.
“MTUWASA imeshika nafasi ya 8
kati ya mamlaka 25 nchini mwaka huu kulingana na ripoti ya EWURA, ni
moja ya mamlaka zinazofanya vizuri. Hivyo, hamna budi kutoka asilimia 60
ya huduma mnayotoa sasa na kufikisha asilimia 100, ili kuendana na
mahitaji ya wananchi pamoja na viwanda vikubwa vilivyopo mjini hapa”,
alisema Katibu Mkuu.
Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa
ili kuendana na Sera ya Viwanda huduma ya maji haina budi kuwa ya
uhakika na endelevu, na MTUWASA inabidi wahakikishe Serikali inafanikiwa
kufikia lengo hilo kama watoa huduma wa maji.
Aidha, aliwaasa wananchi wa
Mtwara kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji, kwani pamoja na juhudi za
Serikali za kuwekeza katika miradi mikubwa ya maji, itakuwa ngumu
kufanikisha lengo la kutoa huduma ya uhakika na endelevu ya majisafi na
salama kama vyanzo vya maji havitatunzwa na kuwa endelevu.
Naye Mkuregenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA),
Inj. Mashaka Sitta alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha mamlaka hiyo
inakuwa bora nchini ndani ya miaka miwili; baadhi ya mipango yao ikiwa
ni kutunza vyanzo vya maji, kuongeza mitandao ya miundombinu ya maji,
kuongeza uzalishaji na wateja ili kufikia lengo hilo.
No comments:
Post a Comment