Mashindano Makubwa ya Afrika ya kuhifadhi na kusoma Qur-an tukufu yanayoandaliwa na Alhikma Foundation chini ya uratibu wa Nurdin Kishiki na mlezi wake Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi yamefikia kileleni leo hii baada ya kupatikana kwa mshindi wa mashindano hayo kwa juzuu 30.
Mshindi huyo kijana wa miaka 12 kutokea nchini Somalia Mohamed Abdullah Aden ametangazwa mshindi kutokana na umahiri wake wa kusoma Qur-an na amekabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 15 kutoka benki ya Amana, milioni 1 kutoka ofisi ya mkoa, IPOD, na fursa ya kutembelea nchi yeyote duniani.
Akizungumzia ushindi wake kijana huyo amesema amefarijika sana, huku akitoa wito kwa waislamu kupendelea kujifunza kitabu kitukufu cha Qur-an.
Mashindano hayo ya 18 yameongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, pamoja na ujumbe kutoka Saudi Arabia uliomuwakilisha Sheikh Mkuu wa Msikiti wa Makkah na Madina Abdul Rahman Al Sudas, na viongozi wengine wa kitaifa na kimataifa akiwemo balozi wa Kuwait, Rais Mstaafu awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais Mstaafu awamu ya nne Gharib Bilal, Katibu Mkuu wa CCM Alhaj Abdurahman Kinana, Muft Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuber na Shekh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum.
Katika Mashindano hayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Meya wa Manispaa ya Temeke Abdallah Chaurembo kuambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo John Mbaga kuhakikisha wanafanya uthamini wa eneo ambalo Alhikma Foundation wanataka kuongeza upanuzi kwa ajili ya huduma za kijamii, ikithibitika halina utata wapewe ruhusa mara moja, huku akihitaji kupelekewa taarifa hizo siku ya Jumanne ofisini kwake
No comments:
Post a Comment