• Breaking News

    ..

    ..

    Wednesday 28 June 2017

    SERIKALI YAJIPANGA KUKUZA LUGHA YA KISWAHILI

    KAMUSI
    Na Zawadi Msalla-WHUSM
    Serikali imeahidi kuweka misingi madhubuti ya kukuza lugha ya Kiswahili kwa kuhakikisha lugha hiyo inatumika katika ngazi mbalimbali ikiwemo kufundishia katika taasisi za kielimu, Mahakamani na Bunge.
    Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Harrison Mwakyembe wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya kuzaliwa kwa Idhaa ya Kiswahili BBC yaliyofanyika katika ukumbi wa Kilimanjaro-Hyatt Regency jana Jijini Dar es Salaam.
    Mhe. Mwakyembe ameeleza kuwa Wizara yake ipo katika hatua za ukamilishaji wa kuundwa kwa sera mpya ya Lugha ambayo itasimamia matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili na kufanya matumizi ya lugha hiyo kukuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
    “Serikali imejipanga kukifanya kiswahili kuwa kati ya lugha tatu bora duniani,kwa sasa ni miongoni mwa Lugha 10 maarufu kati ya Lugha 6000  na Lugha ya pili kutumika barani Afrika” alieleza Waziri Mwakyembe.
    Aliongeza kwa kueleza kuwa uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili utachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa lugha hiyo adhimu  huku Serikali ikihakikisha Kamusi hiyo inasambazwa katika maeneo yote muhimu zikiwemo ofisi zote za Balozi  za Tanzania nje ya nchi, Taasisi za Elimu kuanzia ngazi za awali hadi za juu na mahakamani .
    Vilevile Mhe. Mwakyembe amewapongeza wafanyakazi na uongozi wa Idhaa ya Kiswahili BBC kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Lugha ya Kiswahili inatumika katika matangazo yao na kukifanya kusikiwa dunia kote.
    Aidha Waziri Mwakyembe alitoa wito kwa watanzania wote kukipenda na kukienzi Kiswahili kwani ndiyo kitu pekee kinachoweza kumtambulisha kila mtanzania mahali popote pale duniani

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI