• Breaking News

    ..

    ..

    Monday, 10 July 2017

    Angella Kairuki, aibua mapya ziarani

    Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, ameanza ziara yake Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo kuzifahamu changamoto mbalimbali za watumishi na kutoa maelekezo ya kutatua kero hizo.
    Katika ziara yake ambayo ameanza na Wilaya ya Temeke Waziri Kairuki ameagiza uanzishwaji wa vituo vya kusaidia upatikanaji wa huduma kwa wakati maarufu kama 'One Stop Center' katika  idara ya Mamlaka ya Mapato (TRA) na idara ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ili kuongeza ufanisi wa kazi na ukusanyaji wa kodi kwa wakati, halkadhalika uwepo usajili wa biashara kwa haraka ambapo itasaidia katika Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania maarufu kama “MKURABITA”
    "Hizi One Stop Center ni muhimu sana baadhi ya Mikoa imeanza kunufaika na uanzishwaji wake ikiwemo Mkoa wa Morogoro ambapo imepelekea ukusanywaji wa mapato kwa haraka na kuchochea shughuli za maendeleo" alisema Waziri Kairuki.
    Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ametoa msisitizo kwa Maafisa Utumishi kuhakikisha serikali inapotoa vibali vya kazi, hawaajiri watu bila kujiridhisha na taarifa zao za kielimu ili kuepuka suala la watumishi wenye vyeti feki, ambapo ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa iliyowakilishwa na Katibu Tawala Msaidizi Michael Mungaya wa Mkoa wa Dar es Salaam imeeleza kuwa watumishi 937 wanavyeti feki na katika hao 421 wameleta vyeti pungufu, ni vyema umakini  ukafanyika ili kuondoa hasara kwa taifa.
    Waziri Kairuki ameongeza kuwa  mfumo wa taarifa za watumishi (Lawson) utasaidia katika kuhakiki taarifa zao ikiwemo kujua mahala walipo watumishi  na wanafanya nini, hivyo kupitia mfumo huo watajiridhisha na kufanya maamuzi sahihi kwa watumishi.
    Pia Waziri Kairuki amewasihi watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi bila ya ubaguzi wa aina yeyote na kutenda haki kwa kufanya kazi kwa weledi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, halikadhalika kuepuka suala la kutoa au kupokea rushwa.
    Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Felix Lyaniva amemuomba Waziri Kairuki kuhakikisha kuwa watumishi wanapewa makazi jirani na vituo vyao vya kazi ili kuboresha ufanisi kazi na uwepo wa usalama na ulinzi, pia DC Lyaniva amemueleza Waziri Kairuki kuwa wameweza kuongeza saa limoja la ziada la kuwahudumia wananchi katika wiki ya utumishi wa umma iliyofanyika tarehe 16 mpaka 23 mwezi June.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI