Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imefuta adhabu dhidi ya wanafamilia
wanne waliofungiwa kushiriki masuala la soka kwa mwaka mmoja.
Wanafamilia hao ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa, James
Mwakwinya; Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa
(RUREFA), Blassy Kiondo; Kaimu Katibu wake, Ayoub Nyaulingo pamoja na
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.
Haji Manara alitiwa hatiani
Aprili 23, mwaka huu kwa makosa ya lugha chafu na za chuki kwa viongozi
wa TFF na kupotosha umma dhidi ya kadi njano ya mchezaji Mohammed Fakhi
wa Kagera Sugar ambako alifungiwa kushiriki masuala ya mpira kwa mwaka
mmoja na faini ya Sh milioni tisa.
Viongozi wa RUREFA walifungiwa
kwa mwaka mmoja na faini ya Sh. milioni mbili kwa kila mmoja kwa makosa
ya kukiuka maagizo ya viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliyotaka
wasitishe mchakato wa uchaguzi mkoa kwa kuwa kulikuwa na rufaa
iliyokatwa TFF.
Akizungumza na Wanahabari leo
Julai 17, 2017 Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Tarimba Abbas,
alisema viongozi hao wamesamehewa adhabu zao kwa kuwa waliomba kupitiwa
upya kwa mashauri yao na kamati imeona ni bora kuwaachia huru ili
kuendeleza masuala ya soka.
“Wapo wengi waliofungiwa wengine
maisha na wengine adhabu fupi, msamaha huu ni kwa wale ambao wameomba tu
kupitiwa upya kwa adhabu zao, pia milango ipo wazi kwa wengine ambao
wanataka kupitiwa kwa mashauri yao, lakini si kwa wale waliopanga
matokeo uwanjani,” alisema Tarimba.
Kadhalika, Tarimba aliwaomba
viongozi wa TFF kuandaa semina ya Maofisa Habari na Viongozi wa Ligi Kuu
na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ili kuepuka maneno machafu ambayo
yanasababisha wao kufungiwa.
“Inaonekana viongozi na Maofisa
Habari hawana maneno mazuri ya kuongea na wadau wa soka na ndio maana
matatizo ya kufungiwa yanajitokeza mara kwa mara, naamini wakipata
semina hiyo itawasaidia kujirekebisha na kupunguza kesi kama hizo,”
alisema Tarimba.
Kwa niaba ya TFF, Ofisa Habari wa
Shirikisho, Alfred Lucas, wameyapokea mapendekezo hayo kutoka kwa
Tarimba na kwamba tutafanyia kazi ili kurekebisha makosa hayo kwa
manufaa ya soka la Tanzania.
No comments:
Post a Comment