• Breaking News

    ..

    ..

    Monday, 10 July 2017

    HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA CHINI YA RC MAKONDA WANUFAISHA WAKAZI 80, 000 DAR

                             NA  LUGENZI KABALE
    AKIITIKIA agizo la Rais John Pombe Magufuli
    alilowataka wateule wake kuwa wabunifu na kujituma ili kuwaondolea wananchi
    shida mbalimbali , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametatua
    migogoro takribani 8, 000 iliyowahusisha zaidi ya watu 80, 000 ndani ya
    takribani miezi minane kati ya Disemba mwaka jana na Mwezi Juni mwaka huu.
    Makonda ametekeleza jukumu hilo kupitia timu
    ya wanasheria 35 wanaojitolea kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa
    wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam.
    Kiongozi wa timu ya Wanasheria hao, Georgia
    Kamina, aliitaja baadhi ya migogoro ambayo timu yake imekuwa ikisuluhisha
    kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni ile ya
    umiliki wa ardhi na michakato ya mirathi mahakamani na katika ngazi ya familia,
    Migogoro mingine ambayo timu hiyo ya
    wanasheria imekuwa ikimsaidia Makonda kuitatua kwa kushirikiana na Wakuu wa
    wilaya ya Ilala  (Sofia Mjema), Kinondoni (Ally Hapi), Temeke
    (  Felix Lyaniva ), Ubungo (Kisare Makori ) na Kigamboni
    (_Hashimu Mgandilwa ) ni pamoja na  ndoa na matunzo ya watoto kwa ndoa
    zilizo sambaratika,  ajira na mikataba ya ajira, ubakaji, faili kupotea
    mahakamani, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani, umiliki wa nyumba,  umiliki
    au mauziano ya ardhi, mikopo kutoka mabenki ya biashara, uuzwaji mali
    mbalimbali kwa kukiuka sheria au makubaliano na hata ukosefu wa uaminifu.
    Akiiongea kwa niaba ya Makonda, Kamina
    aliliambia Habari LEO katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni
    katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa,  Ilala Boma Jijini Dar es Salaam hivi
    karibuni, alitaja migogoro wanayopokea na  inayotia fora katika mkoa wa
    Dar es Salaam  kuwa ni ile inayohusisha masuala ya mirathi, umiliki wa
    ardhi, ajira na mikataba kati ya waajiri na waajiriwa, ndoa na matunzo ya
    watoto kwa ndoa zilizo sambaratika na baadhi ya wananchi kuingia mikataba
    mibovu na mabenki katika harakati za kupata mitaji ya biashara.
    “Mheshimiwa Paul  Makonda alichukua
    jukumu la kuanzisha huduma ya msaada wa  kisheria bure kwa wananchi
    kutokana na uzoefu alioupata katika ziara ya kukutana na wananchi aliyofanya
    mkoa mzima mwezi Novemba mwaka jana,” alibainisha Kamina na kuongeza kuwa
    ili kuwaepusha wananchi na mchakato mrefu na unaoumiza wa kumaliza migogoro yao
    mahakamani aliamua kuunda timu ya wanasheria wa kujitolea ili kutekeleza
    dhamira hiyo ya kuwasaidia wananchi wenye migogoro mbalimbali ya kisheria.
    Kiongozi wa timu ya wanasheria hao aliongeza
    kwa kusema kuwa Mkuu wa Mkoa aliguswa na namna baadhi ya wananchi walivyokuwa
    wakipoteza mashamba, nyumba, mali na hata kufukuzwa kazi kwa uonevu kwa kukosa
    uelewa wa sheria.
    “Ili kupata suluhisho la matatizo hayo hapo
    juu na kwakuwa yeye binafsi akiwa msaidizi wa Rais kwa mkoa wa Dar es Salaam
    basi ndio akaja na wazo la kuanzisha kitengo cha kutatua migogoro ya kisheria
    kwa njia ya kutoa huduma ya msaada kisheria bila malipo kwa wananchi katika
    kila wilaya ya mkoa wa Dar es Salaam.
    “Tupo jumla ya wanasheria 35 ambao
    tumegawanyika katika Wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam yaani  Ilala,
    Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni. Tukiwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya
    nilizotaja tunafanya kazi nao kwa karibu sana na pengine wakati mwingine
    tunajumuika na  Makatibu Tawala  wa Wilaya husika (DAS) na hata
    wakati mwingine Wakurugenzi Watendaji wa manispaa za mkoa wa Dar es Salaam
    katika kutatua migogoro hiyo kisheria,” alifichua Mkuu huyo wa Timu ya
    Wanasheria.
    Akizungumzia uzoefu waliopata katika kipindi
    cha miezi saba walichofanya kazi ya kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure
    kwa wananchi kwa kusuluhisha migogoro mbalimbali wamegundua wananchi
    wengi ama hawana au wana uelewa mdogo wa sheria na kila wakati wanafanya makosa
    makubwa ya kisheria yanayoishia kuwaumiza kimaisha.
    “Kuna kina baba na kina mama wengi tu
    wamekuja mara baada ya kunyang’anywa nyumba zao na mabenki kutokana na kukubali
    kutoa hati za nyumba hizo kudhamini mikopo ya jamaa zao wakiamini kuwa kama
    kutakuwa na kutokuelewana kati ya mabenki na ndugu zao nyumba hizo hazitauzwa
    jambo ambalo sio kweli,” alisimulia Kamina.
    Akitaja baadhi ya migogoro iliyowagharimu muda
    na juhudi za ziada kuisuluhisha, Kamina alitaja mgogoro wa umiliki wa ardhi ya
    hekari 28 unaomhusisha Ogwari Nashon na wakazi wa kijiji cha Viwege, Mbondela
    eneo la Chanika katika Wilaya ya Ilala.
    “Mgogoro huu ulifika mahala ukahatarisha
    maisha ya ndugu Nashon kwani baadhi ya wanakijiji wasioheshimu sheria walivamia
    eneo lake, kuchoma moto majengo na kuharibu mazao kama mihogo, mananasi na
    michungwa.
    Mara baada ya Nashon kuja ofisi ya Mkuu wa
    wilaya ya Ilala alikutanishwa na wanasheria wa  Mkuu wa Mkoa
    wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria  bure kwa wananchi walioko
    wilayani hapo na kueleza tatizo lake ambapo timu yetu iliingilia kati  kwa
    kushirikiana na Mkuu wa wilaya ya Ilala Sofia Mjema, ili kupata ufumbuzi wa
    mgogoro huo.
    Ni jambo la kutia faraja kwa sasa tumepiga
    hatua kubwa kuelekea kutatua mivutano iliyokuwepo kwani Nashon ana vielelezo
    halali vya nyaraka za kiserikali zinazothibitisha umiliki wa eneo hilo,”
    alibainisha Kamina.
    Licha ya kujitokeza picha nzuri iliyojaa mafanikio ya huduma hii
    ya msaada wa kisheria kwa wananchi   katika  Mkoa wa Dar es
    Salaam, Habari Leo imearifiwa juu ya changamoto lukuki zinazowakabili watoa
    huduma hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
    Baadhi ya changamoto hizo ni wananchi kutokuwa na uelewa wa
    sheria, kanuni na taratibu za kukopa fedha kwa watu binafsi na katika taasisi
    za fedha, wananchi hawana uelewa wa sheria na taratibu za mirathi na hata
    wasimamizi wa mirathi hawajui wajibu wao kwa warithi na kwa mahakama jambo
    ambalo linapelekea warithi kuchelewa au kutopatiwa haki zao hata baada ya
    mchakato wa mirathi kukamilika katika Mahakama.
    “Katika eneo la ajira huko ndio kunatisha kwa uvunjaji wa sheria
    za ajira na nchi uliokithiri kwani makampuni mengi hasa ya ujenzi na ulinzi
    hayatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, wakati mwingine mikataba inakuja
    kutolewa baada ya mwajiriwa kuwa amekwisha fanya kazi muda mrefu na inapotolewa
    inakuwa inakiuka makubaliano ya awali,” alisema na kuwanyooshea kidole viongozi
    wa serikali za mitaa na kata, katika baadhi ya maeneo kwa kuwa chanzo cha
    migogoro kwa kufanya majukumu ambayo si yao kisheria na uendeshwaji wa kesi
    mahakamani kuchukua muda mrefu pasipo na sababu za msingi huku Mabaraza ya kata
    nayo kuwa dhaifu katika kutekeleza majukumu yake ya kimsingi katika kuwahudumia
    wananchi na hasa wale wa kipato cha chini.
    Akizungumzia huduma hiyo, Makonda alisema aliamua kuanzisha
    huduma ya msaada wa kisheria kupitia wanasheria hawa (35) katika kila wilaya ya
    mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala
    Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoagiza kusikiliza na kutatua kero au malalamiko
    ya wananchi.
    Mkuu huyo wa Mkoa alifafanua kuwa katika ziara ya mkoa wa Dar es
    Salaam mwishoni mwa mwaka 2016 aligundua  wananchi wengi hawakuwa na
    uelewa wa sheria jambo lililowafanya kupoteza haki zao aidha kwa kutapeliwa,
    kuonewa au kutojua mahala sahihi pa kupeleka matatizo hayo.
    “Pamoja na changamoto nyingi zinazoambatana na huduma hii
    ya kutafuta suluhu ya matatizo ya wananchi kwa kuzileta pande husika mezani
    kuongea bado nina dhamira ya kuendelea kuwasaidia Watanzania wenzangu kwa
    juhudi na maarifa yangu yote.
    Na hii ndio gharama ya kuteuliwa na Rais,
    unapoteuliwa na Mkuu wa nchi anakuwa na matarajio mengi kutoka kwako. Mimi
    nimeamua kufanya ninayoweza kwa nguvu na juhudi zote ili kumuondolea Rais John
    Pombe Magufuli na mashinikizo juu ya shida mbalimbali za Wana Dar es
    Salaam,” alimaliza Makonda

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI