Ripoti mpya iliyotolewa Alhamis
wiki hii na Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF, imesema upatikanaji
wa huduma za msingi za maji na zenye kusimamiwa vema zimeimarika nchini
Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hivi
sasa nchini Tanzania, mtu 1 kati ya 2, au Watanzania milioni 27 wanapata
huduma za msingi za maji—kwa maana ya kwamba zinapatikana ndani ya
mwendo wa dakika 30 kwenda na kurudi kuteka maji ukiwemo muda wa kupanga
mstari.
Hata hivyo, bado kuna kasi ndogo
ya maendeleo katika usafi wa mazingira na mwili kwani asilimia 63 ya
Watanzania hawana huduma bora za kujifanyia usafi.
Ulimwenguni kote, walau watu 3
katika 10 au watu bilioni 2.1 hawapati maji salama na kwa kiasi cha
kutosha nyumbani na watu 6 katika 10, au watu bilioni 4.4 hawana huduma
za usafi zinazosimamiwa kwa usalama.
Ripoti ya Programu ya Usimamizi wa Pamoja, Maendeleo
katika Huduma za Maji ya Kunywa, Usafi wa Mazingira na Mwili: Taarifa
Mpya za 2017 na Kigezo cha Lengo la Maendeleo Endelevu (Progress on Drinking Water, Sanitation and Hygiene: 2017 Update and Sustainable Development Goal Baselines), inaonyesha tathmini ya kwanza ya ulimwengu ya huduma za maji ya kunywa na usafi “zinazosimamiwa kwa usalama”.
Katika ngazi ya ulimwengu, ripoti inaonyesha kwamba mabilioni ya watu wamepiga hatua katika kupata huduma za msingi
za maji ya kunywa na usafi wa mazingira tangu mwaka 2000, lakini huduma
hizi si lazima kwamba zinatoa maji na mazingira safi yaliyo salama.
Makazi mengi, vituo vya afya na shule nyingi bado hazina sabuni na maji
kwa ajili ya kunawa mikono. Jambo hili linaziweka afya za watu
wote—hasa watoto wadogo—katika hatari ya kupata magonjwa, kama vile
kuhara.
Matokeo yake, kila mwaka kote
ulimwenguni, watoto 361,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 wanakufa kwa
kuhara. Huduma duni za maji, usafi wa mazingira na mwili (WASH)
zinaendelea kuathiri uwezekano wa kuishi na afya ya watoto. Nchini
Tanzania, asilimia 8 ya vifo vya watoto chini ya miaka 5 vinasababishwa
na kuharisha ambao ni ugonjwa unaozuilika.
“Siyo tu kwamba usafi duni,
kujisaidia popote, na ukosefu wa maji salama na mifumo ya usafi ndiyo
vyanzo vikuu vya magonjwa na vifo vya watoto, bali yanachangia pia
katika utapiamlo na kudumaa, na haya yanakuwa vikwazo kwa elimu ya
wasichana na fursa za kiuchumi kwa watu maskini,” alisema Maniza Zaman,
Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania. “Takwimu hizi mpya zinatoa picha
halisi na kuonyesha tofauti kubwa kabisa za ukosefu wa usawa wenye haki,
ikiwemo nchini Tanzania, kwa maana ya nani ananufaika na huduma za maji
salama na usafi. Huu ni wito wa kuanzisha vuguvugu la kitaifa ambalo
kweli litaimarisha huduma za maji, usafi wa mazingira na wa mwili ili
kwamba kila mmoja afikiwe hasa katika maeneo yaliyo nyuma, jamii maskini
kabisa na watoto walio hatarini sana, wakiwemo watoto wenye ulemavu,”
aliongeza.
Ripoti inazidi kufafanua kwamba
bado kuna ukosefu wa usawa kati ya jamii za vijijini na mijini. Kwa
mfano, nchini Tanzania, ni asilimia 37 tu ya wakazi wa vijijini
wanaopata huduma bora za msingi za maji (mwendo wa dakika 30 kwenda na
kurudi) kulinganisha na asilimia 80 ya wakazi wa mijini.
Akizungumzia umuhimu wa maji na
usafi kwa afya bora, Dkt. Matthieu Kamwa, Mwakilishi wa WHO nchini
Tanzania anasema, “Upatikanaji wa maji salama na usafi wa kutosha
unachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha ubora wa maisha na
uzalishaji kwa ajili ya maendeleo endelevu. Lengo la SDG la 6 linatoa
wito wa kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na usimamizi endelevu wa
maji na usafi kwa wote. Ni wito mtukufu wa kuleta hakikisho kwamba hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma kama kanuni muhimu ya kufikia kila lengo lililoainishwa katika SDGs”.
Hakujawahi kuwepo hapo kabla haja
kuu ya kutetea haki za kupata maji, usafi wa mazingira na mwili kwa
raia wote na hasa kwa watoto wetu kama ilivyo sasa. Uwekezaji,
uanzishwaji ushirika, uchukuaji hatua madhubuti na uwajibikaji mkubwa
unaosukumwa na data ili kuleta matokeo unahitajika ili kwamba haki hii
ya msingi ifanyike kweli kwa wote.
No comments:
Post a Comment