Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa
kampuni ya Hari Singh & Sons, Jaspal Singh (kushoto), wakati
akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Chuo Kikuu yenye urefu wa KM 2.6 kwa kiwango cha lami, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kampuni ya Hari
Singh & Sons, Jaspal Signh, akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, kuhusu maendeleo ya
ujenzi wa barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Chuo Kikuu yenye urefu wa KM 2.6 kwa kiwango cha lami, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kimara Baruti – Msewe – Chuo Kikuu yenye urefu wa KM 2.6 inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambapo ujenzi wake umefika asilimia 57.
Mhandisi wa miradi kutoka Wakala
wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Ngusa Julius, akimuonesha Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, ramani ya
Daraja la Mlalakuwa lenye urefu wa mita 15 kila upande linalojengwa na
Kampuni ya Milembe & Kika JV eneo la Kawe, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa
Kampuni ya Milembe & Kika JV anayejenga Daraja la Mlalakuwa lenye
urefu wa mita 15 kila upande, lililoko barabara ya Mwai Kibaki, wakati
akikagua ujenzi wake, jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa sehemu ya chini ya
ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa lenye urefu wa mita 15 kila upande,
lililoko barabara ya Mwai Kibaki, jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………….
Serikali imetoa siku 60 kwa
mkandarasi wa Kampuni ya Hari Singh & Sons kumaliza ujenzi wa
kipande cha barabara cha kilomita 1.5 kilichobaki kwa kiwango cha lami
katika barabara ya Kimara Baruti-Msewe-Chuo Kikuu yenye jumla ya urefu wa kilomita 2.6.
Akitoa agizo hilo jijini Dar es
salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa anamaliza mradi huo
haraka na kwa viwango vilivyo kwenye mkataba ili idumu kwa muda mrefu.
“Ikifika mwezi Oktoba nataka unikabidhi barabara hii ikiwa
imekamilika kwa kiwango cha lami na vigezo vinavyokubalika, amesisitiza
Eng. Ngonyani.
Aidha, Naibu Waziri Ngonyani
amefafanua kuwa mkandarasi huyo hatoruhusiwa kutekeleza mradi mwingine
wa barabara nchini endapo atashindwa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo
kwa wakati.
Kwa upande wake Mhandisi Mradi
kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Ngusa Julius, amesema
kuwa TANROADS tayari imeshatoa notisi kwa mkandarasi huyo kuwa kama
hatakamilisha kazi ya ujenzi ndani ya muda wa mkataba hatua za kudai
fidia kulingana na mkataba zitafuata na baadae kukatisha mkataba.
Ameongeza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unasimamiwa
na TANROADS kupitia kitengo chake cha wahadisi washauri wazalendo (TECU)
na unagharimu shilingi Bilioni 5.7 ikiwa ni fedha za Serikali kwa
asilimia mia moja.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Eng. Ngonyani amekagua daraja la Mlalakuwa lenye urefu wa mita 15
kila upande, lililopo barabara ya Mwai Kibaki jijini Dar es salaam na
kusisitiza kwa mkandarasi Milembe & Kika JV kuhakikisha anamaliza
ujenzi wa daraja hilo kwa wakati.
Ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa unagharimu shilingi Bilioni 4.8 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwakani
No comments:
Post a Comment