Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub
Muhammed Mahmoud, amesema kazi iliyoko mbele kwa sasa ni kutekeleza
maagizo yaliyotoolewa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein wakati wa ziara yake
katika mkoa huo.
Alieeleza kuwa
wajibu wa kutekeleza maagizo hayo si jambo la hiyari na kwamba kila
mtendaji katika ngazi zote anapaswa kufanya kazi aliyopangiwa kwa kasi
ile ile anayoitaka Mhe. Rais.
“Ni
lazima tuhakikishe tunakwenda kwa kasi inayotakiwa na kama kuna mtu
asiyeweza kuendana na kasi hiyo ni bora akae pembeni,” alisisitiza
Ayoub.
“Sasa ni wakati
wa kazi tu na uzembe sasa mwiko, na watakaozembea hatutawafumbia macho
wala kuwaonea muhali. Ninafanya hivi kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais
ambao ni wajibu wangu kikazi,” aliweka bayana.
Aidha alisema
miongoni mwa changamoto atakazozishughulikia ni msongamano wa magari
katika maeneo ya Mji Mkongwe, uchangiaji damu kwa hiyari, kutokomeza
malaria na kuwakamata watu wanaokaidi marufuku ya kuingiza wanyama
maeneo ya mjini.
Kuhusu tatizo la
idadi kubwa ya wanafunzi maskulini, alisema ujenzi wa madarasa
uliozinduliwa hivi karibuni kupitia kampeni ya ‘Mimi na Wewe’
unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano uliopo kwa sasa
baada ya kukamilika ujenzi huo ambao pia unafanyika katika skuili
nyengine ikiwemo Sharifu Msa.
Alieleza kuwa,
wingi wa wanafunzi katika darasa moja ambapo katika baadhi ya skuli
hufikia 160, haukumfurahisha Mhe. Rais, ambapo alipongeza juhudi za
ujenzi wa madarasa mapya unaofanyika kwa nguvu za wananchi chini ya
uongozi wa mkoa huo.
Baadhi ya miradi
iliyotembelewa na Dk. Shein katika ziara yake mkoani humo, ni ule wa
kuhifadhi mazingira katika bahari ya Kilimani ambapo maji yamekuwa
yakipanda hadi katika maeneo ya makaazi ya wananchi.
Aidha alifungua
jengo la Chuo cha Utalii Maruhubi, ujenzi wa barabara ya Kinuni, nyumba
za kisasa Fumba na Nyamanzi na mradi wa maji safi na salama Bumbwisudi
na pia alifungua skuli ya Kihinani.
Dk. Shein pia alitembelea uwanja wa Mao Tse Tung unaofanywa na wataalamu kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Wakati huohuo,
Mkuu wa Mkoa alipokea hundi ya shilingi 15,000,000 kutoka kampuni
inayotoa huduma za kiufundi mijini na vijijini (Urban and Rural
Engeneering Service Company) yenye ofisi zake Mikocheni jijini Dar es
Salaam.
Fedha hizo
zilizotolewa na Naibu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Salum Mussa Omar, ni
kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa madawati kwa skuli za msingi Mkoa
wa Mjini Magharibi.
No comments:
Post a Comment