YANGA SC imetoka nyuma na kushinda mabao 3-2 dhidi ya Singida
United katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Shujaa wa Yanga katika mchezo wa leo alikuwa ni kiungo mshambuliaji,
Emmanuel Martin aliyefunga bao la ushindi kwa shuti la umbali wa mita 23
baada ya pasi ya mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.
Singida walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa 2-1, mabao yote matatu yakifungwa na wachezaji wa kigeni kipindi cha kwanza.
Kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko alianza kuifungia Yanga bao la
kwanza dakika ya tano kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya mshambuliaji
mpya, Ibrahim Hajib kuangushwa umbali wa mita 25.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda kwa misimu yote miwili
iliyopita, Dany Usengimana akaifungia Singida United bao la kusawazisha
dakika ya nane akitumia vizuri makosa ya nabeki wa Yanga kuchanganyana.
Mshambuliaji Mzimbabwe, Simbarashe ‘Simba’ Nhivi Sithole akaifungia bao
la pili Singida dakika ya 23 akitumia tena makosa ya safu ya ulinzi ya
Yanga.
Kipindi cha pili, kocha Mzambia wa Yanga alibadilisha karibu kikosi
kizima akimtoa hadi kipa Beno Kakolanya na kumuingiza Mcameroon, Yoouth
Rostand.
Mabadliko hayo yaliisaidia Yanga kupata mabao mawili dakika za mwishoni,
akianza Mrundi Tambwe kusawazisha kwa penalti dakika ya 83 baada ya
kipa Said Lubawa kumchezea rafu kiungo chipukizi, Said Juma, kabla ya
Martin kufunga la ushindi dakika yab 90 na ushei.
Katika mchezo huo, Singida walipoteza mikwaju miwili ya penalti, wa
kwanza dakika ya kwanza kabisa Elisha Muroiwa akipaisha juu ya lango na
ya pili, kipa Rostand akiokoa shuti la pembeni la mshambuliaji Atupele
Green.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Beno Kakolanya/Youth Rostand, Juma Abdul,
Hajji Mwinyi/Hassan Kessy, Kevin Yondan/Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’/Abdallah Hajji ‘Ninja’, Thabani Kamusoko, Pius
Buswita/Emmanuel Martin, Raphael Daudi/Juma Mahadhi, Donald Ngoma/Amiss
Tambwe, Ibrahim Hajib/Said Juma na Baruan Akilimali.
Singida United; Said Lubawa, Michael Rusheshagonga, Shafiq Batambuze,
Elisha Muroiwa, Juma Kennedy, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Tafadzwa
Kutinyu, Nhivi Simbarashe, Danny Usengimana na Kigi Makas
No comments:
Post a Comment