Sehemu ya vijana wa Kijiji cha
Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma
wakishiriki kazi ya kuchimba Lambo kwa kutumia nguvu zao wenyewe.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii
Bw. Patrick Golwike akishiriki kuchimbua eneo la Lambo la Kijiji cha
Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mpwapwa Bw. Mohamed Maje akiweka mchanga kwenye ndoo katika
zoezi la uchimbaji wa Lambo Kijijini cha Manghungu.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha
Manghungu, kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma
wakishiriki kazi ya kuchimba Lambo kwa kutumia nguvu zao wenyewe.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii
Bw. Patrick Golwike akikabidhi nyundo nzito kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji
cha Manghungu, kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma
Bw. Sospeter G. Nyaombo kuwezesha kazi ya uchimbaji wa Lambo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii
Bw. Patrick Golwike akikabidhi jembe kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha
Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw.
Sospeter G. Nyaombo kuwezesha kazi ya kuchimba Lambo la maji kijijini
hapo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii
Bw. Patrick Golwike akikabidhi chepeo kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha
Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw.
Sospeter G. Nyaombo wakati wa kushiriki uchimbaji wa lambo kijijini
hapo.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha cha
Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw.
Sospeter G. Nyaombo akionesha moja ya ndoo zilizotolewa na Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia Wazee na watoto kuwezesha kazi ya
uchimbaji wa Lambo.
Mratibu wa masuala ya Maendeleo ya
Jamii kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bibi Mwajina Lipinga akijumuika
na akinamama kuimba wimbo wa kuhamsha ari ya kuchimba Lambo la maji ya
kunywa wakati alipotembelea Kijiji cha Manghungu ,Kata ya Vinghawe
Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
……………………………………
Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Serikali imeadhimia kuwa Sera
ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, inatekelezwa kikamilifu na
inafuatilia utekelezaji wa Sera hiyo katika ngazi ya mikoa, Wilaya, Kata
na Vijiji mbalimbali hapa nchini.
Akiongea na wananchi wa Kijiji cha
Manghangu, kilichoko Kata ya Vinghawe Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma,
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amesema
Sera hiyo imeweka wazi kuwa wananchi ndiyo kitovu cha maendeleo maana
ushiriki wao unatoa dhamana thabiti ya maendeleo na ustawi wa wananchi
katika ngazi mbalimbali.
Bw. Patrick Golwike ametanabaisha
kuwa lengo la kufika katika Kijiji hicho ni kushirikiana na wananchi
kufanya kazi za maendeleo kwa vitendo.
“Kazi ya kuhamsha ari iliyobuniwa
na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalenga
kuhamasisha wananchi kushiriki katika kuibua miradi, kupanga, kutekeleza
na kusimamia shughuli za maendeleo kwa kutumia rasilimali zilipo katika
mazingira yao ili kujiletea maendeleo yao” alisema Bw. Golwike.
Kwa upande wake Mratibu wa masuala
ya Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bibi Mwajina
Lipinga, alisema kuwa mradi wa ujenzi wa lambo la maji, na ushiriki wa
wananchi katika kazi za kujitolea utakuwa chachu kwa vijana kuhamsha ari
ya kujitolea na kuchangia maendeleo ya vijiji na Taifa.
“Kazi hii inayofanyika naomba iwe
chachu kwa mikoa mingine ipende kuhamsha ari na kwa kufanya kazi kama
kipimo cha heshima na utu wa mtu” alisema Bibi Lipinga.
Aliongeza kuwa, wananchi wanapoona
Serikali na wadau wanajitokeza kusaidia kufanya kazi fulani, jamii
nayo inawajibu wa kujitokeza katika kushughulikia changamoto zilizopo
ili kupata majawabu yenye ufumbuzi wa matatizo hayo kwa manufaa ya
wanachi wote.
Akiongea katika zoezi la uchimbaji
wa lambo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwapwa Bw. Mohamed A. Maje
ameahidi kuendeleza kazi ya kushirikiana na jamii katika kutekeleza
miradi ya maendeleo kwa kutumia nguvu za wananchi.
“Nitaandaa matukio mengine mawili
ya kuamsha ari ya wananchi kufanya kazi za maendeleo yao ambayo
yatasimamiwa na Halmashauri ili kurejesha ushiriki wa wananchi katika
kazi za kujitolea” alisema Bw. Maje.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha
Manghangu Bw. Sospeter G. Nyaombo alishukuru Wizara kwa kufika kijijini
na kutoa msaada wa vifaa vya uchimbaji wa Lambo pamoja na kushirikiana
kazi kwa vitendo.
“Kufika kwenu katika kijiji chetu
kumekuwa chachu ya kuchangia maendeleo katika kijiji chetu na maeneo
mengine nchini” alisema Bw.Nyaombo.
Vifaa vilivyotolewa na Wizara ni pamoja na majembe 27, chepeo 5, nyundo 3, na ndoo 10.
Mradi wa uchimbaji wa Lambo la
maji safi umekadiriwa kukamilika katika kipindi cha siku 15. Chanzo hiki
cha maji kitanufaisha kaya zipatazo 538, wananchi 2297, kati yao
wanaume wakiwa 983 na wanawake 1314
No comments:
Post a Comment