Kaimu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM) Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
Septemba 7, 2017 Amezindua Programu maalumu kwa Vijana wa CCM katika
ushiriki wa shughuli za miradi ya Kimaendeleo, Kiuchumi na Kijamii
katika ukumbi wa CCM (NEC) Mjini Dodoma.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo Shaka alisema Wazo hilo limeibuliwa wakati
muafaka huku serikali ya CCM awamu ya tano chini ya Mwenyekiti wa CCM na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli
ikiweka mkazo na vipaumbele kadhaa vinavyomtaka kila mtanzania hususani
vijana kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha Mali.
Alisema
dhana ya kufanya kazi kwa bidii, malengo na shabaha si ngeni lakini kwa
wakati huu inahubiriwa kwa nguvu kulingana na changamoto nyingi
zilizopo, fursa, ushirikishwaji kwa kuzingatia mahitaji halisi kutokana
na mabadiliko ya dunia Kiuchumi na Kimaendeleo.
Aliwasisitiza
Vijana kutambua wajibu wa kukuza shughuli za kazi na maisha zikiongozwa
na nguvu ya uzalendo, kujali utaifa na kutambua dhamana iliyopo ya
kudumisha amani, Umoja, Mshikamano na Maendeleo.
“Ili
kusihi yote hayo hatimaye Vijana waweze kuyafanikisha tunapaswa kuwa na
mioyo isiyopwaya au kukosa rutuba ya kutodumisha uzalendo, tunalazimika
kwa pamoja kutambua mpango wowote wa kuyafikia maendeleo ya kweli
utabaki ni hadithi na ndoto Kama hatutaongozwa na shime ya uzalendo au
kutothamini utaifa wetu Kama ambavyo viongozi wanatuhimiza siku Hadi
siku” Alisema Shaka
Shaka
aliwaeleza Vijana kuwa pamoja na kuwepo juhudi kubwa za mara kwa mara
kuchukuliwa na serikali, mashirika hiari ya Kijamii na yasiyokuwa ya
kiserikali, kuelimisha juu ya dhana ya ushirikishwaji na ushiriki wa
Vijana katika miradi ya Kiuchumi na Kijamii wanapaswa kuwa na utayari,
uthubutu, uzalendo, na Utaifa.
Alisema
kuwa Vijana wanapaswa kukubali kujadiliana na wenzao juu ya mpango wa
maendeleo na hatma ya Taifa na mustakabali wake kwani ndiyo njia pekee
ya kukuza uzalendo kwa Taifa.
Alisema
mataifa yaliyoendelea yametokana na watu wake kukubali kufanya kazi
kwani Ndiko kuliko yakomboa mataifa hayo yaliyoendelea kutoka katika
uchumi duni na kuhamia katika uchumi wa Kati na Sasa wakionekana kuwa na
uchumi wa maendeleo ya viwanda.
“Mafanikio
hayakuja Kama zawadi kwenye kisahani Cha Chai ama kutokea kwa bahati
mbaya Kama mtende unavyoota jangwani ni lazima kukubali kwa pamoja
kufanya kazi ili kupambana na adui umasikini”
“Wakati
huu ambao serikali imebeba mzigo wa kutoa elimu bure toka msingi Hadi
sekondari ni lazima Vijana tuwe na muktadha mmoja wa kujenga mtazamo wa
pamoja kwa kujitambua na kukubali kufanya kazi bila kusukumwa” Alisema
Shaka
Aliongeza
kuwa kazi ya Vijana siku zote na kila wakati inapaswa kuwa ni kufikiri,
kupambanua, kubuni na kujadiliana ili kumaliza changamoto, vikwazo,
fursa na matumizi ya nafasi husika katika Jamii.
Aidha,
kupitia kusanyiko hilo aliwaagiza na kuwataka makatibu wote wa Umoja wa
Vijana wa CCM wa mikoa na Wilaya nchini kila mmoja kuhakikisha programu
hiyo inaanzishwa katika mikoa na Wilaya zake na kusisitiza kuhitajika
matokeo makubwa kwani ataandaa utaratibu wa kuthamini programu hiyo kila
kipindi Cha robo mwaka.
Sambamba
na hayo pia Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi Ndg Shaka Hamdu Shaka alishiriki ujenzi wa shule ya Msingi
Mizengo Pinda iliyopo katika Kijiji Cha Chinangali 2 Kata ya Bwigili
Wilayani Chamwino.
Pamoja
na kushiriki shughuli ya uchimbaji msingi, ufyatuaji tofali na
matengenezo ya tungilizi kwa ajili ya upauaji wa majengo ya shule hiyo
pia Shaka alichangia mifiko 20 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono
juhudi za wananchi walizozianza kwa kujitolea nguvu, muda na rasilimali
zao.

No comments:
Post a Comment