NCHI za Marekani na Uingereza zimeingilia kati mvutano wa kisiasa
unaoendelea baina ya Chama cha Jubilee na Muungano wa Vyama vya Upinzani
(NASA) kuhusu uchaguzi wa Rais nchini Kenya kwa kuzitaka pande
zinazohusika ziondoe masharti waliyoweka na zizungumzie kupata mwafaka.
Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec na Naibu Balozi wa
Uingereza nchini humo, Susie Kitchens wamekaririwa wakisema kuwa,
uchaguzi wa marudio usipofanyika Oktoba 26 mwaka huu, kutakuwa na
mgogoro wa kikatiba kwenye nchi hiyo. Mwishoni mwa wiki, Katibu wa
mgombea urais kupitia Nasa, Dennis Onyango alisema mwanasiasa huyo Raila
Odinga na mabalozi walizungumzia masuala kadhaa, lakini kubwa zaidi ni
mvutano kuhusu uchaguzi wa marudio wa Rais, muswada wa mabadiliko ya
sheria za uchaguzi na kinachoendelea katika Tume Huru ya Uchaguzi na
Mipaka ya Kenya (IEBC).
Wanadiplomasia hao wamekaririwa kusema kuwa, masharti mengi yaliyotolewa
hayatekelezeki kwa kuwa muda hautoshi. NASA wametoa masharti kadhaa
likiwemo la kufukuzwa kwa maofisa 10 wa IEBC akiwemo Ofisa Mtendaji
Mkuu, Ezra Chiloba. NASA pia wanataka zabuni zilizotolewa kwa kampuni ya
Al-Ghurair inayochapisha karatasi za kupigia kura, na kampuni ya
masuala ya teknolojia ya Safran Morpho zisitishwe.
Muungano huo pia unashinikiza muswada wa mapendekezo ya marekebisho ya
sheria za uchaguzi yaliyowasilishwa bungeni kwa pendekezo la Jubilee
yaondolewe. NASA wamesema, kama masharti yao hayatatekelezwa
hawatashiriki kwenye uchaguzi Oktoba 26 na wataandamana kila Jumatatu na
Ijumaa kushinikiza yatekelezwe.
Kiongozi wa chama chenye wabunge wengi katika Bunge la Seneti, Kipchumba
Murkomen, amesema, wanadiplomasia hao wanataka uchaguzi ufanyike kwa
amani na mwanasiasa yeyote asifanye vurugu Mgombea Mwenza wa Uhuru
Kenyatta kwenye uchaguzi wa Rais, William Ruto amesema mgombea urais
kupitia muungano huo, Raila Odinga hana mamlaka ya kuzuia Wakenya
wasipige kura Oktoba 26, mwaka huu.
Amemtaka Raila aache kuwapotosha Wakenya kwamba uchaguzi hautafanyika
siku hiyo. Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi,
Raila alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria za uchaguzi ni
kuishambulia demokrasia na Katiba hivyo lazima yapingwe.

No comments:
Post a Comment