Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya
Amali, imesema madai ya walimu juu ya maslahi mazuri, lazima yaende
sambamba na utekelezaji wa majukumu yao ya ufundishaji kama inavyopasa.
Naibu Waziri wa wizara hiyo Mmanga
Mjengo Mjawiri, amesema ufundishaji usiokidhi viwango ni miongoni mwa
sababu kadhaa zinazoshusha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Akizungumza leo Oktoba 8, 2017
katika kongamano lililofanyika kwenye ukumbi wa Sanaa Rahaleo kwa ajili
ya kuadhimisha ‘Siku ya Walimu Duniani, Mjawiri alisema walimu wengie
hawayamudu masomo wanayofundisha.
“Ili mwalimu aweze kufahamika
vizuri na wanafunzi wake, lazima kwanza alijue vyuema na alimudu somo
lake ili fundishe kwa ufasaha na ustadi mkubwa,” alifahamisha.
Aidha, Naibu Waziri huyo alisema
walimu wana wajibu wa kuzingatia misingi mikuu ya ufundishaji, mbinu na
maadili ili kufikia malengo yanayotakiwa.
Alisema mbinu na uweledi
unahitajika wakati wa kufundisha ili kuwawezesha wanafunzi wote, wale
wenye uwezo mkubwa wa ufahamu na walio wazito, ili kuwafanya wanafahamu
na kwenda sambamba na mwalimu.
Mjawiri alikumbusha kuwa, lengo la
‘Siku ya Walimu Duniani’, ni kuwatanabahisha umuhimu wa kujitathmini,
kujifahamu na kujikosoa ili wafanikiwe katika jukumu la ulezi na
ufundishaji walilokabidhiwa.
Aidha alieleza kuwa wizara yake
imeweka utaratibu wa kutembelea skuli mbalimbali kwa lengo la kufahamu
maendeleo ya wanafunzi pamoja na mpango mzima wa ufundishaji .
Alisema utaratibu huo utasaidia
kufahamu viwango vya walimu katika kufundisha, na hivyo kuzipatia
ufumbuzi changamoto hizo na nyengine zinazokabili skuli hizo.
Hata hivyo, alisema tayari baadhi
ya changamoto zimeanza kupatiwa ufumbuzi ikiwemo wingi wa wanafunzi
unaosababisha msongamano na hivyo kuwafanya walimu kutosomesha kwa
uhuru, utulivu na ufanisi.
Changamoto nyengine alizosema
zimeanza kutatuliwa, ni malimbikizo ya posho za likizo wanazodai
walimu, vifaa vya kufundishia na uhaba wa walimu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu
wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) Salim Ali Salim, alisema chama
hicho kinapaswa kutumia fursa ya kipekee kutathmini utekelezaji wa
mapendekezo yaliyotolewa mwaka 1996 na Shirika la Kazi Duniani (ILO)
pamoja na UNESCO, kuhusu hadhi ya kazi ya ualimu.
Walimu walioshiriki kongamano hilo
wameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa jitihada zake za
kuhakikisha changamoto za kimaslahi, uhaba wa vifaa na mafunzo
zinarekebishwa kadiri uwezo unavyopatikana.
Kaulimbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya Siku ya Walimu Dunaini, ni “Uhuru wa Ajira ya Walimu Humjenga Mwalimu.”
No comments:
Post a Comment