Akizungumza kwa nyakati tofauti
wakati wa ziara yake kutembelea Chama cha Walimu, Idara ya Mahakama na
Jeshi la Polisi nchini jana, Naibu Waziri alieleza kuwa tatizo la mimba
kwa watoto wa kike mashuleni limekuwa kubwa na kuathiri sio tu maendeleo
yao bali taifa kwa jumla.
‘’Tatizo hili ni kubwa na athari
zake si kwa wasichana tu wanaolazimika kuacha shule na kupoteza fursa ya
kuendelea na masomo bali hata kwa taifa kwa kuwa linatunyima wasomi na
wataalamu wa kuendeleza nchi yetu”Alisema Naibu Waziri.
Alibainisha kuwa mwaka 2012
wasichana takriban 2,400 kwa shule za msingi pekee walipata ujauzito
ingawa idadi hiyo alieleza kuwa imekuwa ikipungua ambapo mwaka jana
wasichana 250 wameripotiwa kupata ujauzito. Hata hivyo, alieleza kuwa
tatizo hilo linaonekana kuwa kubwa zaidi kwa upande wa Sekondari.
Naibu Waziri alieleza kuwa
kuongezeka kwa tatizo la mimba kwa wasichana mashuleni kunachangiwa na
kuporomoka kwa maadili katika jamiii, baadhi ya mila na desturi,
kuongezeka kwa matumizi ya simu za kisasa (smartphone) na vishawishi
vingine.
Aidha, alibainisha kuwepo kwa
ukiukwaji mkubwa wa sheria unaofanywa na Mahakama, Jeshi la Polisi
pamoja na Chama cha Walimu kwa kuwateteta baadhi ya watumishi
wanaohusika na vitendo vya kuwapa mimba wasichana hivyo kutoa wito wa
watumishi kuacha mara moja mwenendo huo na kutaka sheria zifuatwe
ipasavyo.
“Mwaka jana bunge lilipitisha
sheria kali kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa kike,
anatakiwa kupewa adhabu ya kufungwa jela miaka 30, mtu yeyote
anayemkatisha masomo mtoto wa kike, yaani anayemuozesha, anayewezesha,
anayeshabikia, anayefungisha ndoa wakiwemo wazazi Masheikh, Mapadre ama
walezi nao pia wanapaswa kufungwa miaka 30,” alisisitiza Naibu Waziri
Kakunda.
Aidha alisema kuwa mahakama,
polisi pamoja na wazazi wamekuwa hawalichukulii kwa uzito suala hili
kwani rushwa ndogo ndogo hususani ngazi za halmashauri bado zimeendelea
kuongeza ukubwa wa tatizo hilo hivyo ametoa wito kwa mahakama pamoja na
polisi kulivalia njuga jambo hilo ili kuwanusuru na kuwaokoa watoto wa
kike dhidi ya janga la kupata mimba hapa nchini.
“Kuna baadhi ya watendaji wa
vijiji, kata, walimu wakuu waliopo chini ya halmashauri wamekuwa
wakipatanisha kesi hizi nje ya utaratibu, mfano mkosaji anaweza
kulipishwa ng’ombe, fedha au hata mbuzi kesi inaisha hivyo tu, kwa hiyo
nikuombe Jaji kiongozi upeleke msukumo mkubwa kwa watumishi wa mahakama
na Jeshi la Polisi katika ngazi za halmashauri ili waweze
kulishughulikia suala hili kwa mujibu wa sheria,” alisistiza Naibu
Waziri Kakunda.
Kwa upande wake Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu Ferdinand Wambali alisema kuwa mahakama inatambua kuna
changamoto katika utekelezaji wa sheria hususani mazingira ya kutungwa
kwa sheria hiyo, utekelezaji wake lakini pia ushirikiano kutoka kwa
wananchi.
“Sheria nyingi zinatungwa lakini
wananchi wengi haziwafikii katika hali ya kawaida, hivyo unaweza kuona
kuwa makosa yanaendelea ni kwa sababu wananchi hawajaelewa haswa nini
kinachopaswa kufanywa, lakini pia wananchi hawaelewi hata namna ya kutoa
ushirikiano kwa kutoa ushahidi kwa baadhi ya makosa ya jinai kwa polisi
na mahakama,” alisema Jaji Wambali.
Kwa upande wake, Msaidizi wa IGP
Simon Sirro, Kamishna Mussa Ali Mussa kutoka makao makuu ya polisi,
alisema kuwa tatizo hilo linafanyiwa kazi kwa ukaribu zaidi na polisi
kwa kushirikiana na jamii ambapo mpaka sasa baadhi ya mambo
wameshayafanya ikiwemo kuanzisha dawati la jinsia kwa vituo vya polisi
katika halmashauri mbalimbali kwa lengo la kukabiliana na changamoto
hizo.
“Katika mfumo wa ushirikishwaji
tulionao, tumeteua askari mmoja kwa kila kata ili huyu askari
akashirikiane na kamati ya ulinzi ya kata kutatua kero mbalimbali
zilizopo ndani ya kata ikiwemo watoto wa kike kupata ujauzito wakiwa
shuleni,” alieleza Kamishna Mussa.s
Naibu Waziri Kakunda ambaye
aliteuliwa hivi karibuni alifanya ziara hiyo ili kushauriana namna bora
ya ushirikiano kati ya wizara yake na taasisi hizo kupunguza kama si
kutokomeza kabisa tatizo mimba za wasichana mashuleni
No comments:
Post a Comment