MKUU wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi
Evarist Ndikilo akipokelewa kwa mabango na baadhi ya watu ,wakati
alipokwenda mradi wa reli ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam-
Morogoro inayojengwa na kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkezi ya nchini
Uturuki ,huko Soga wilayani Kibaha.
Mwakilishi wa kampuni ya Yapi
Merkezi ya nchini Uturuki ,inayojenga mradi wa reli ya Standard Gauge
kutoka Dar es Salaam- Morogoro,Mhandisi Mert Oz ,(aliyesimama katikatika
)akimuonyesha maelezo yaliyomo kwenye karatasi,mkuu wa mkoa wa Pwani
,Mhandisi Evarist Ndikilo(wa kwanza kushoto) wakati alipokwenda
kutembelea mradi huo huko Soga wilaya ya Kibaha.
Picha na Mwamvua Mwinyi
…………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi
Evarist Ndikilo amewasimamisha watumishi wawili wa kampuni ya ujenzi ya
Yapi Merkezi ya nchini Uturuki inayojenga reli ya Standard Gauge kutoka
Dar es Salaam- Morogoro kwa tuhuma za rushwa ya ajira.
Aidha ameagiza watumishi hao wasimamishwe kupisha uchunguzi huku akitoa siku saba kwa vyombo vya dola kufuatilia suala hilo.
Mkuu huyo wa mkoa ,aliyasema hayo wakati alipotembelea ujenzi wa mradi huo kwenye kijiji cha Soga wilayani Kibaha .
Mhandisi Ndikilo,alieleza kuwa endapo ikibainika wamehusika na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aliwataja watumishi hao ambao
walikuwa wakilalamikiwa na wananchi waliokuwa wakienda kuomba kazi kuwa
walikuwa wakiomba rushwa ni pamoja na Nelson ambae ametambulika kwa jina
moja ofisa mwajiri (HR) kwenye kampuni hiyo .
Mwingine ni Torong’ong’o ambaye ni dereva wa moja ya viongozi wa kampuni hiyo ambao hawakuhudhuria hata kwenye mkutano huo.
Awali mhandisi Ndikilo alipokelewa
kwa mabango na watu waliokuwa nje ya kampuni hiyo wakilalamika kunyimwa
ajira upande wa madereva na waendeshaji wa mitambo wakidai kuwa ajira
zinatolewa kwa njia ya rushwa.
“Tunanyimwa ajira hasa tunaotoka maeneo ya Kibaha na mkoa wa Pwani kwa ujumla na wanaoajiriwa ni watu wa nje ya mkoa”walisema.
Mhandisi Ndikilo,alielezea kwamba
alikuwa pia akipelekewa malalamiko ofisini kwake ambapo baadhi ya
madereva waliandika majina yao na kuambatanisha vyeti vyao na uzoefu wao
wa kazi lakini hawakupata ajira.
“Malalamiko yamekuwa ni mengi sana na wanaolalamika wanasema
wamenyimwa ajira wengi ni wa hapa Kibaha na mkoa wa Pwani ambao
walipaswa kunufaika na mradi huu kwani kila eneo lenye mradi lazima
wahusika wa eneo wapewe kipaumbele “
“Inadaiwa walioajiriwa hata 100 hawafiki katia ya 390 ya walioajiriwa,” alisema Ndikilo.
“Tumeambiwa kuna baadhi wanaajiriwa kusikojulikana wakija hapa
wanaingizwa moja kwa moja na kati ya wafanyakazi 390 wengi wanatoka nje
ya mkoa huku wa hapa wakiambulia kula vumbi tu wakishinda hapa nje bila
ya mafanikio,” alisema mhandisi Ndikilo.
Akizungumzia suala hilo Diwani wa Kata ya Soga Ramadhan Chezeni
alisema taarifa kuwa wapo watu wameajiriwa kwa kufuata sifa si la
kweli.
Alieleza kuna vijana wengi wanasifa zinazostahili lakini wanasumbuliwa bila ya kupata ajira.
Kwa upande wake Meneja mradi huo uliochini ya Reli Assets
Holding Company (RAHCO) ,mhandisi Maizo Mgedzi alisema suala la rushwa
halifahamu .
Alisema anachojua wanaoajiriwa wote ni wenye sifa na vigezo ,na wanatoka nchini bila ya kujali eneo analotoka.
Mgedzi alisema kuwa watahakikisha
wanalifuatilia suala hilo ili kupisha uchunguzi lengo likiwa ni
kuhakikisha hakuna malalamiko kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi
huo.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Yapi
Merkezi Mhandisi Mert Oz alisema,endapo watabaini wapo walioingizwa
kwenye ajira kinyume cha utaratibu,hawatasita kuwaondoa.
Oz alisema , wanafuata taratibu za ajira na wanategemea kuletewa wafanyakazi kwa utaratibu wa nchi na kufuata sheria za ajira.
No comments:
Post a Comment