Mamlaka ya chakula na dawa TFDA
imezifutia usajili dawa mbalimbali za kutibu magonjwa ya binadamu na
kuziondoa kwenye soko pamoja na kusitisha matumizi yake kutokana na
kuwa na madhara makubwa kwa wagonjwa.
Hayo yameelezwa jana Jijini
Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti Sillo, alipokuwa akifungua
mafunzo ya siku tano ya wakufunzi wa ufuatiliaji juu ya ufundishaji
na uhamasishaji wa masuala ya udhibiti wa madhara yatonayo na matumizi
ya dawa zisizosalama kwa watendaji wa afya kutoka Wilaya zote za mkoa
wa Arusha.
Bw. Sillo mesema katika kudhibiti
matumizi ya dawa zisizofaa TFDA imeondoa dawa ya sindano aina ya
Chloramphenical kwenye soko baada ya shirika la afya Duniani WHO,
kubaini dawa hiyo ina madhara kwa watumiaji, Pia mamlaka hiyo imefuta
usajili wa dawa zingine kama vile Ketoconazole, (vidonge)
Phenylpropanalamine,Dextropropoxyphene,Nimesulide,stavudine 40,
Gatifloxacin,Rofecoxib, pamoja na Celecoxib baada ya kuthibitika zina
madhara kwa watumiaji.
Aidha matumizi ya dawa kama vile
Kanamycin,Amikacin na Levofloxacin zimebadilishwa ili ziweze kutumika
kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa kifua kikuu pekee.
Mkurugenzi huyo wa TFDA amesema
mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi 60 nchini kote na yanafanyika
katika mikoa mbalimbali yakiwashirikisha Madaktari, Manesi, na
wafamasia walioko kwenye hospitali, vituo vya afya na Zahanati.
Bw.Sillo alieleza kwamba, lengo
la mafunzo hayo ni kuongeza idadi ya wakufunzi wa masuala ya usalama wa
dawa kutoka 73 hadi 133 na tayari katika kipindi cha miaka mitatu
2014/ 15 hadi 2017/18, Mamlaka ya chakula na dawa imehamasisha watendaji
wa afya wapatao 2000 nchini kote na sasa uhamasishaji unaendelea
katika mkoa wa Katavi.
Alisema mara baada ya mafunzo
hayo wakufunzi hao watafundisha wenzao kwenye maeneo yao ya kazi ili
kuongeza uelewa kwa wataalam wengi zaidi kufahamu taratibu zilizoko
za udhibiti wa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa zisizofaa.
Aliwakumbusha wakufunzi hao
kwamba kila mtendaji wa afya ana wajibu wa kulinda afya za wagonjwa
anao watibu au kuwahudumia na wajibu huo ni pamoja na kuhakikisha
wagonjwa wanabaki salama na ikiwa watapata madhara hatua za kuwatibu
zinachukuliwa na kutoa taarifa ili kuzuia kusambazwa zaidi kwa dawa
zinazoleta madhara.
Bw. Sillo alifafanua kuwa,
kumekuwa na baadhi ya wataalam wa afya kudhani kuwa kwa kutoa taarifa
kuwa dawa ina madhara inaonekana kuwa wao ndio wanaosababisha madhara
hayo na kusisitiza kuwa dhana hiyo sio ya kweli, hivyo akawasisitiza
watoe taarifa sahihi ili wananchi wafahamu madhara yatokanayo na
matumizi ya dawa pamoja na hatua za kuchukua.
Mamlaka ya chakula na dawa kwa
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma wametengeneza mfumo wa
kielektroniki wa utoaji wa taarifa za usalama na madhara ya dawa
ambao ulizinduliwa Oktoba 2016 na Waziri wa afya Mh.Ummy Mwalimu.
Kabla ya kuzinduliwa mfumo huo
taarifa za usalama na madhara ya dawa zilikuwa zikitolewa kwa kutumia
fomu maalumu za njano ,kijani na blue ambapo watoa huduma za afya
walikuwa wakitumia fomu za njano huku wagonjwa wakitoa taarifa kwa
kutumia fomu za za kijani, na fomu za bluu zilitumika kutoa taarifa za
ubora wa dawa na kama kuna dawa duni au bandia kwenye soko.
No comments:
Post a Comment