Serikali imesema kuwa
utekelezaji wa mpango wa Kilimo Kwanza umekuwa na mafanikio katika
uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini ambapo uzalishaji wa
jumla wa mazao ya biashara katika msimu wa mwaka 2016/2017 umeongezeka
kufikia Tani 881,583 ukilinganisha na Tani 796,562 katika msimu wa mwaka
2015/2016.
Naibu Waziri wa Kilimo
Mhe Mary Mwanjelwa amebainisha hayo Leo Novemba 7, 2017 Bungeni Mjini
Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi
Mkoani Singida Mhe Yahaya Omary Masare aliyetaka kufahamu Kuna mafanikio
kiasi gani kwa mazao ya biashara na chakula kwani Katika mpango wa
kilimo Kwanza serikali ilihamasisha watanzania kuongeza uzalishaji
katika kilimo ili serikali itoe mikopo ya matrekta.
Mhe Mwanjelwa alisema
kuwa mafanikio ya mpango huo ni makubwa kwani Katika Wilaya ya Manyoni
uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kufikia Tani 42,554 katika
msimu wa mwaka 2015/2016 ambapo uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka
Tani 1342 mwaka 2011/2012 hadi kufikia Tani 6212 mwaka 2015/2016.
Alisema kwa upande wa
Zao la Alizeti uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 4464 mwaka 2010/2011
hadi kufikia Tani 21,871 mwaka 2016/2017 wakati huo huo zao la Ufuta
uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 2285 mwaka 2010/2011 hadi kufikia
Tani 8874 katika msimu wa mwaka 2015/2016.
Aliongeza kuwa katika
Mkoa wa Singida uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka Tani
453,297 mwaka 2013/2014 hadi Tani 481,452 mwaka 2015/2016.
Uzalishaji wa mazao ya
biashara umeongezeka kutoka Tani 184,066 mwaka 2012/2013 hadi kufikia
Tani 293,873 katika msimu wa mwaka 2015/2016.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri Mhe Mary Mwanjelwa alisema kuwa Jumla ya Matreka
yanayofanya kazi nchini ni 18,774 ambapo kati yake Matrekta makubwa ni
11,500 na matrekta madogo ya mkono ni 7274.
Alisema kuwa Wilaya ya
Manyoni pekee ina jumla ya matrekta makubwa 32 Matrekta madogo ya Mkono
39 na wanyamakazi 14784 yanayotumika katika kuongeza ufanisi wa kilimo
ambapo pia kilimo cha kutumia Maksai ni maarufu katika Wilaya hiyo.
Alisema kuwa pamoja na
jitihada za serikali kuu katika kuhakikisha wakulima wanapata zana bora
za Kilimo Halmashauri za Wilaya kote nchini zimelekezwa kuhamasisha
wakulima kujiunga au kuanzisha vyama vya akiba na Mikopo (SACCOS)
ambavyo vitakopesha wanachama wake au kuwadhamini kupata mikopo kutoka
kwenye Taasisi za fedha kwa ajili ya kununua Zana hizo bora za Kilimo
ikiwemo Matrekta.
Akijibu swali la
Nyongeza la Mbunge Masare aliyetaka kufahamu namna ya kupatiwa mikopo
kwa wananchi ambao hawajajiunga na vyama vya akiba na mikopo
(SACCOS), Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa alisema kuwa sifa ya
wananchi kukopeshwa ni pamoja na kujiunga na Vyama Vya Ushirika lakini
pia Wizara ya Kilimo kupitia Mfuko wake wa Taifa wa pembejeo za kilimo
ataruhusiwa mkulima mmoja mmoja kukopa jinsi atakavyo kwa kufuata
taratibu zilizowekwa.
No comments:
Post a Comment