Na Frank Mvungi, MAELEZO- Dodoma
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka
Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la
kuupatia maji mji wa Kisarawe uliopo Mkoani Pwani kutoka katika mtambo
wa Ruvu Juu.
Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo
vya Habari iliyotolewa na DAWASA inaonyesha kuwa kazi zilizofanyika hadi
sasa kabla ya zabuni kutangazwa ni pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu
wa kina wa mradi, kuandaa makabrasha ya zabuni na kutangaza zabuni .
“Kwa sasa Kazi ya uchambuzi wa
zabuni zilizowasilishwa na kufunguliwa mwishoni mwa wiki inaendelea
ambapo Kampuni 12 za ndani na nje ya nchi zimejitokeza kuomba kutekeleza
mradi huo” inasisitiza sehemu ya Taarifa hiyo..
Taarifa hiyo imebainisha kuwa
mradi huo mkubwa kwa awamu yakwanza utahusisha ujenzi wa kituo cha
kusukuma maji kitakachokuwa na uwezo wa kusukuma maji kiasi cjha lita 60
kwa sekunde na kujengwa kwa kituo chenye uwezo wa kuhifadhi lita
480,000 za maji.
Mradi huo utahusisha ununuzi na ulazaji wa mabomba makuu kwa umbali wa kilometa17 hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Kisarawe.
Awamu ya Pili itahusisha ujenzi wa
tenki la Vigungu ambalo litahudumia eneo lililotengwa kwa ajili ya
makazi mapya na nyongeza ya maji kwa ajili ya Viwanda vitakavyojengwa.
Aidha DAWASA imechukua hatua za
muda mfupi kupunguza tatizo la maji katika mji huo ikiwemo Wizara ya
Maji na Umwagiliaji kupitia DAWASA kutekeleza mradi wa maji wa Vigama
kwa kuchimba Kisima kipya,Kufunga Pampu, Kujenga mnara, kufunga tenki la
kuhifadhia maji na kulaza mabomba ya kusambaza maji hayo ambapo
mkandarasi wa kutekeleza mradi huo amepatikana na mradi utaanza mwezi
Februari mwaka huu.
Hatua nyingine itakuwa DAWASA
kukarabati kisima cha Shule ya Sekondari Manneromango ikiwa ni mchango
wake katika mkakati wa kuboresha miundo mbinu ya shule ili kuongeza
ufaulu katika Wilaya hiyo,mradi huo utaanza kutekelezwa machi mwaka huu
DAWASA imekuwa ikitekeleza miradi
mbalimbali ya Maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ikiwa ni sehemu
ya jitihada za Serikali kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa
wananchi wake .
No comments:
Post a Comment