Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai amempa pongezi Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza kusikiliza
maoni ya Bunge na wabunge kwa kutekeleza moja ya maombi yao kuigawa
Wizara ya Nishati na Madini.
Ndugai ametoa pongezi hizo leo Januari 8, 2018 akiwa Ikulu jijini Dar
es Salaam katika hafla ya kuapishwa kwa Naibu Waziri wa Madini, Mhe.
Doto Mashaka Biteko na kusema kwa miaka mingi walikuwa wakitaka Wizara
hizo kugawanywa lakini ilikuwa inashindikana ila katika awamu ya tano
Rais Magufuli ndiyo ameweza kufanya hivyo.
"Sisi Bunge tulikuwa tukishauri toka miaka ya nyuma kwa
Serikali kwamba Wizara iliyokuwa inaitwa Wizara ya Nishati na Madini
ilikuwa ni nzito mno, ilikuwa imejaza mambo mengi sana kwa wakati mmoja
ushauri wetu ulikuwa ni vizuri kuzitenganisha na kuzisimika kila moja
kivyake. Jambo hili Mhe. Rais umelitekeleza kabisaa kwenye awamu ya tano
umeunda wizara mbili na hata tendo la leo linadhirisha kabisa jinsi
ambavyo unazidi kuimarisha sekta ya Nishati na Madini kwa hili
tunakushukuru sana kwani linaonesha dhamira yako ilivyo" alisema Ndugai
Mbali na hilo Ndugai amesema kuwa katika miaka ya nyuma katika sekta
ya madini na nishati kama nchi tumeliwa sana hivyo anaamini kuwa katika
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli na wateule wake jambo
hilo halitaweza kuendelea tena.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajiwa kuanza mnamo Januari 30, 2018 Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma

No comments:
Post a Comment