Mbunge mwingine nchini Kenya,
amekamatwa kuhusiana na mzozo unaozunguka kujiapisha kwa aliyekuwa
waziri mkuu Raia Odinga kwa kile anachokitaja kama rais wa watu wa
Kenya.
Mbunge wa Makadara jijini Nairobi George Aladwa alikamatwa
asubuhi ya Jumamosi nyumbani kwake na maafisa wa idara ya upelelezi na
kupelekwa hadi makao makuu ya idara hiyo kwa mahojiano zaidi.Aladwa ambaye amewahi kuwa meya wa jiji la Nairobi, alikuwa katika mstari wa mbele katika mipango ya sherehe hizo ambayo haikuwa na idhini ya serikali.
Aladwa sasa ni mbunge wa pili kukamatwa kuhusiana na hafla hiyo ambayo pia imeshutumiwa na jamii ya kimataifa.
Mbunge mwingine wa Nairobi Tom Kajwang alikamatwa na kufikishwa mahakamani na hatimaye kuachiliwa kwa dhamana.
Mwanaharakati mwingine wa upinzani wakili Miguna miguna pia alikamatwa siku ya Ijumaa na angali anazuliwa na polisi licha ya mahakama kuruhusu kuachiliwa kwake kwa dhamana.
Bwana Aladwa alikamatwa siku ya Ijumaa usiku katika nyumba yake iliopo Buruburu kulingana na kiranja wa walio wachache bungeni Junet Mohamed.
Bwana Mohammed ambaye pia mbunge wa Suna Mashariki alisema kuwa bwana Aladwa kwa sasa anazuiliwa katika makao makuu ya ujasusi.
Polisi hawajatoa tamko lolote kuhusiana na kukamatwa kwa Aladwa.
No comments:
Post a Comment