• Breaking News

    ..

    ..

    Wednesday, 7 February 2018

    Sophia Mjema ametembelea maeneo mbalimbali ya mradi wa DMDP

    Na Stahmil Mohamed
    Mkuu wa wilaya ya ilala Bi. Sophia Mjema leo ametembelea maeneo mbalimbali ndani ya wilaya ya ilala na kukagua maendeleo ya mradi wa DMDP ambao ni mradi wa maendeleo ndani ya jiji la Dar es salaam ambao unahusisha jumla ya wilaya nne ndani ya jiji ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni ambao unategemewa kukamilika februari 27 mwaka huu.
    Akiongea na vyombo vya habari katika ziara hiyo Bi. Mjema amesema kuwa katika mradi huo kutajengwa barabara takribani nne pamoja na jengo moja ambalo litatumika kama maabala kwa ajili ya kupima kokoto na udongo utakaokuwa unatumika katika ujenzi wa barabara hizo lakini pia litatumika kwa ajili ya mikutano ya wahandisi watakaohusika katika ujenzi huo.
    Akitaja barabara zinazojengwa pamoja na gharama zake amesema kuwa ni barabara ya Ndanda yenye kilometa 0.35, barabara ya Ulimpio kilometa 0.86, barabara ya kiungani kilometa 0.70 na barabara ya paruku yenye kilometa 0.40 ambazo kwa ujumla zimegharimu bilioni 11 huku jengo likigharimu bilioni 1.
    Pia amesema kuwa ujenzi wa barabara hizo utasaidia kutatua changamoto ya msongamano wa magari ndani ya jiji kwa sababu barabara hizo zitakuwa zinaunganisha magari moja kwa moja na barabara ya uhuru na kuhakikisha kuwa baada ya barabara hizo kukamilika foleni zitapungua kwa kiasi kikubwa.
    Aidha amesema kuwa pamoja na mradi huo kuendelea vizuri bado kuna changamoto kwa baadhi ya maeneo ambapo wafanyabiashara wanafanya biashara eneo la barabara huku ujenzi ukiwa unaendelea hivyo amewaomba wananchi kupenda barabara zao ili kwa pamoja waweze kufikia lengo kwani itawasaidia hata wao wenyewe kufanya biashara katika mazingira mazuri pasipo na vumbi.
    Pia ameongeza na kusema kuwa wilaya ya ilala itatoa vibanda vya kufanyia biashara katika masoko matatu ya Buguruni, hasa kwa vijana wasiokuwa na kazi maalumu na kuwaomba kufika ofisi za halimashauri ya ilala kuanzia jumatatu ya tarehe 12  na kusisitiza kuwa vibanda hivyo vitatolewa bure bila malipo yoyote.
    Kwa upande wake mhandisi kutoka manispaa ya ilala Mboya  amesema kuwa ujenzi  wa jengo litakalotumika kwa ajili ya vipimo vya kokoto na udongo itasaidia na kuleta ufanisi katika ujenzi wa barabara na kuongeza kuwa itasaidia pia katika majaribio kwani itapelekea kupata matokeo kwa muda mfupi na kazi kutendeka kwa muda muafaka.
    Pia mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Abubakhari Said amesema kuwa wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa kwani umeweza kutatua changamoto ya maji kujaa wakati wa mvua na kuahidi kwamba watashirikiana na serikali kukemea wafanyabiashara wanaoweka biashara zao pembezoni mwa barabara.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI