Na Paschal Dotto-MAELEZO
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Rais Mstaafu (Awamu ya Tatu),
Mhe. Benjamin William Mkapa ametangaza uteuzi wa Profesa Egid Beatus
Mubofu kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, nafasi iliyokuwa
inashikiliwa na Profesa Idris Suleiman Kikula.
Uteuzi huo umetangazwa rasmi leo tarehe 5, Machi 2018 kupitia
taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Mkuu wa UDOM,
Mhe. Benjamin Mkapa.
Kabla ya uteuzi huo Profesa Mubofu alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na kabla ya hapo alikuwa Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi wa Profesa Mubofu unaanza rasmi tarehe 17 Machi, 2018.
Profesa Idris Kikula ni miongoni mwa wanazuoni waandamizi
wanaoheshimika ndani na nje ya nchi kitaaluma kwa kushiriki katika
tafiti mbalimbali za kisayansi na kijamii
Ameshiriki katika tafiti hizo kwa kushirikiana na taasisi nguli za
kitafiti hapa nchini kama REPOA, pamoja na taasisi ya UONGOZI.
UDOM ndio chuo kikuu pekee chenye uwezo mkubwa wa kuchukua
wanafunzi wengi hapa nchini na Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara na
inakadiriwa kina uwezo wa kuchukua wanafunzi takriban 40,000, pia kina
eneo la ukubwa wa hekari zaidi ya 6000
No comments:
Post a Comment