Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ametangaza Vita na Wanaume wanaowapa Ujauzito Wanawake na kuwatelekeza jambo linalopelekea ongezeko la Watoto wa Mitaani, Wadada kufukuzwa nyumbani na wengine kulazimika kuuza Uji, kukaanga Samaki,Mandazi na Vitumbua ili wapate fedha ya kuhudumia Mtoto na kwa ugumu wa maisha hujikuta wanashindwa kulipa Kodi ya Nyumba na kufukuzwa huku Mwanaume akiendelea kula starehe na kuongeza Wanawake.
RC Makonda amesema kitendo cha Wanaume kukwepa majukumu ya malezi na matunzo kwa Mtoto imepelekea pia baadhi yao kutoa Ujauzito, kutupa Watoto na wengine kupeleka wajukuu kulelewa na Wazee na kusababisha mzigo kwa familia.
Kutokana na hilo RC Makonda ameandaa jopo la wanasheria na Maafisa Ustawi wa jamii watakaoanza kuchukuwa hatua za kisheria kwa wanaume wanaokwepa majukumu yao kuanzia April 09 Mwaka huu kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha RC Makonda amesema kuwa wataangalia pia utaratibu wa kufanya marekebisho sheria ya gharama za matunzo ya mtoto kwakuwa ni ndogo na haiendani na hali ya sasa.
Ikiwa leo ni Siku ya wanawake Duniani RC Makonda amesema lengo lake ni kuleta ukombozi kwa kinamama ili kuhakikisha wakihitaji fedha ya matumizi wanapatiwa na sio kupigwa, kusimangwa, kutukanwa na kudhalilishwa.
Hata hivyo Mhe. Makonda amesema atashirikiana na kusimama bega kwa bega na wanawake wote waliotelekezwa kudai haki zao.
Mhe. Makonda ameamua kutoa muda wa mwezi mmoja ili kama kuna Baba kwenye huu Mkoa anajijua ametelekeza Mtoto na hatoi fedha za matunzo akamtafute na kuanza kutoa fedha ya Matunzo kwakuwa itakapofika April 09 na ikithibitisha umetelekeza Mtoto utachukuliwa hatua kali za kisheria.
MWANAUME UNAPOMPA UJAUZITO MWANAMKE UJUE UNALO JUKUMU LA KULEA MTOTO HADI ATAKAPOJITEGEMEA.
No comments:
Post a Comment