Chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Tanzania (TALGWU) kimeishukuru serikali kuwarudisha kazini watumishi walioajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei 2004 ambao waliondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kidato cha nne.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu mkuu TALGWU Rashid Mtima amesema anaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuzingatia mapendekezo yaliyowasilishwa na chama hiko serikalini mnamo tarehe 22 machi mwaka huu.
Amesema mapendekezo waliyowasilisha serikalini ilikuwa ni kuiomba serikali kuwarudisha kazini watumishi wote walioondolewa katika utumishi kwa kukosa sifa ya kuwa na elimu ya kidato cha nne.
Aidha amesema kufikia tarehe 9 april mwaka huu menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora mh. Kapten mstaafu George Mkuchika alitoa kauli ya serikali bungeni Dodoma ya kuwarejesha watumishi hao kazini,walipwe mishahara yao kwa kipindi chote walioondolewa na kuendelea na ajira zao mpaka watakapostaafu kwa mujibu wa sheria.
Pia ametoa pole kwa wanachama na watumishi wote ambao waliondolewa katika utumishi wa umma kimakosa na waajiri wao kwa kigezo cha kuwa na elimu ya darasa la saba.
Hata hivyo Mtima amesema baadhi ya waajiri katika halmashauri mbalimbali katika kutekeleza agizo la menejimenti ya umma ya kuwaondoa watumishi hao walifanya tafsiri potofu na kuwaondoa watumishi wenye elimu ya darasa la saba walioajiriwa kabla ya tarehe 20 mei 2004 na kupelekea wanachama 7,382 kuondolewa kazini.
No comments:
Post a Comment