KOCHA Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez amesema hasira zote za kufungwa na Simba katika mchezo uliopita, atazihamishia katika mchezo dhidi ya Ndanda FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara kesho.
Katika mchezo uliopita Azam FC ilifungwa na Simba Taifa bao 1-0 na kuvunja rekodi yao ya kutopoteza mchezo hata mmoja, tangu kuanza kwa msimu huu mpya wa Ligi Kuu Tanzania bara. Hernandez aliliambia gazeti hili kuwa kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinaibuka na ushindi katika mchezo huo wa ugenini.
“Tumesikia Uwanja wa Nangwanda sio mzuri, lakini tumejipanga kuhakikisha tunatumia mipira mirefu kupata ushindi. Ni lazima tubadilishe aina ya uchezaji wetu kupata matokeo mazuri,” alisema.
Kocha huyo alisema kuwa jambo la muhimu amekuwa akiwaandaa wachezaji kurudisha nguvu na kujipanga upya kwa mchezo huo, baada ya kutumia nguvu nyingi katika mchezo uliopita.
Azam FC ilitarajiwa kuwasili Mtwara jana tayari kwa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania bara, ikiwa tayari imeshacheza michezo mitano, ikishinda mitatu dhidi ya Mbeya City 2-1, dhidi ya Tanzania Prisons 1-0, dhidi ya Majimaji 3-0, ikipata sare ya bao 1-1 dhidi ya African Lyon na kufungwa na Simba 1-0.
Timu hiyo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 10 sawa na Yanga inayoshika nafasi ya pili huku Simba ikiongoza kileleni kwa pointi 13.
Azam ilipokutana na Ndanda FC katika mchezo wa kwanza msimu uliopita kwenye uwanja huo wa Nangwanda Sijaona, ilishinda bao 1-0, na iliporudiana baadaye Dar es Salaam zikatoka sare ya mabao 2-2.
No comments:
Post a Comment