MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imesema fao la kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii, na kwamba, lilifutwa tangu mwaka 2012.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa, pamoja na kufutwa kwa fao hilo, kutokana na malalamiko mengi, hivi sasa ipo kwenye majadiliano na kukusanya maoni ya wadau kuhusu fao hilo, ili serikali itoe uamuzi muafaka utakaonufaisha pande zote.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Irene Isaka, ametoa msimamo huo wakati alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu utendaji wa mamlaka hiyo na suala la fao la kujitoa.
Amesema kutokana na tamko hilo la serikali, mamlaka hiyo ilifanya utafiti na tathmini mbalimbali na sasa iko katika hatua ya kukusanya maoni na baadaye itafanya majadiliano ya utatu; serikali, mamlaka hiyo na wafanyakazi ili kupata muafaka.
Isaka amesema tayari baadhi ya mifuko imeanzisha mafao mbadala kama vile fao la matibabu, uzazi, ulemavu na ajali ambayo yanatumika kumsaidia mwanachama kwa kumpunguzia gharama za maisha yake.
Mwanasheria wa Mamlaka hiyo, Ansgar Mushi, amesema kwa sasa mifuko yote ya pensheni ina wanachama milioni 2.1 kati yao, mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii wapo wanachama milioni 1.1 wakati mfuko wa bima ya afya wapo wanachama 920,701.
Aidha, alisema mpaka sasa mifuko hiyo ina wastaafu 105,057, michango ya wanachama hao inayofikia Sh trilioni 1.69 na bima ya afya Sh bilioni 88.5, ambayo jumla yake ni Sh trilioni 1.78.
No comments:
Post a Comment