Mgeni rasmi katika uzinduzi wa
jiko la umeme-jua, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa
ya Moshi, akisikiliza maelezo ya namna jiko hilo linavyofanya kazi
kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa Kituo cha Zana za
Kilimo na Teknolojia Vijijini – CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi.
Kushoto kwa Noela ni mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices Moshi,
Farida Makame. Wengine pichani ni washiriki wa kikundi hicho. Uzinduzi
wa jiko hilo lililotengenezwa na CAMARTEC kwa ufadhili wa Green Voices
ulifanyika hivi karibuni mjini Moshi.
Jiko la umeme-jua ambalo
limetengenezwa na CAMARTEC kwa ufadhili wa mradi wa Green Voices
Tanzania kwa ajili ya kikundi cha akinamama wa TAWOCA Moshi. Jiko hilo
linafaa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa
mazingira.
Wanakikundi wa TAWOCA Green
Voices Moshi wakihakikisha jinsi joto la jua linavyosaidia kupika kwa
kutumia jiko la umeme-jua. Kushoto ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa
jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi.
Picha ya pamoja.
…………………………………………………….
VIUNGA vya ukumbi wa Aroma mjini
Moshi vimesheheni akinamama wengi katika siku hii ya Jumamosi, kama
ilivyo kawaida kwa siku kama hiyo, ambapo wote wanaonekana kuwa na nyuso
za furaha kutokana na mijadala inayoendelea.
Lakini tofauti na Jumamosi
nyingine ambapo akinamama wa kikundi cha Wamama wa Kahawa ambao ni
wanachama wa Tanzania Women Coffee Association – TAWOCA mjini humo
kujadili masuala mbalimbali ya ujasiriamali, siku hii inaonekana kuwa ya
tofauti kwa sababu licha ya idadi ya akinamama kuongezeka, lakini kuna
tukio kubwa na muhimu ambalo limewakutanisha.
“Leo tunazindua rasmi jiko la
umeme-jua, yaani parabolic solar cooker, ambalo kupitia udhamini wa
mradi wa akinamama wa Green Voices, hatimaye limeweza kupatikana baada
ya jithada za miezi kadhaa,” ndivyo anavyoanza kuelezea Farida Makame,
mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices wa kikundi hicho, huku
akionyesha kifaa kinachofanana na dish kama la satellite ambacho
katikati yake kumewekwa sufuria inayong’aa kama taa kubwa ya umeme.
Anasema kwamba, jiko hilo
linaweza kupika kila aina ya chakula kwa kutumia mionzi ya jua ya moja
kwa moja bila kuathiri mazingira.
“Kwa kutumia jiko hili maana yake
huhitaji kutafuta mkaa wala kuni, hivyo kuokoa misitu ambayo inateketea
kila siku kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kutafuta nishati ya
kupikia,” anaongeza.
Farida, ambaye pamoja na
akinamama wengine 14 – wakiwemo wanahabari watano wanawake – walipatiwa
mafunzo ya takriban miezi miwili jijini Madrid, Hispania mapema mwaka
huu wa 2016, anasema kwamba lengo la kubuni na kutengeneza jiko hilo la
umeme-jua ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kupambana
na uharibifu wa mazingira.
Anaeleza kwamba, haikuwa kazi
rahisi kwake kukamilisha ubunifu wake, wazo ambalo aliliwasilisha akiwa
mafunzoni, na kwamba ndiyo maana mradi wake umechelewa kutokana na
kuhitaji teknolojia zaidi.
“Tumeanzisha huu mradi baada ya
kukaa na akinamama wa TAWOCA na kuwauliza changamoto mbalimbali
zinazowakabili katika maisha yao, moja ya changamoto ni upatikanaji wa
kuni na mkaa, gesi na umeme.
“Kwahiyo tukaangalia kama kuna
njia mbadala ambayo akinamama wanaweza kuitumia na ikawa nafuu na pia
kiafya, kwa sababu njia ya kutumia umeme-jua ina manufaa sana kiafya,
kwa hiyo tukaungana na wenzetu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia
Vijijini, CAMARTEC, kwa sababu ndio watafiti wa mashine na zana za
kilimo, ili kutengeneza jiko hili linalotumia nishati ya jua,” anasema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Uhawilishaji Teknolojia wa CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi anasema
imekuwa ni fursa kubwa kwao kufanya kazi na mradi wa Green Voices, kwani
wameweza kutengeneza kwa mara ya kwanza jiko hilo ambalo limewapa
hamasa wahandisi wa kituo hicho kuliboresha zaidi kwani linaonekana kuwa
na manufaa makubwa.
Anakiri kwamba, ingawa wanabuni
teknolojia mbalimbali ikiwemo kutengeneza majiko na makaushio
yanayotumia umeme-jua, lakini hiyo ndiyo mara ya kwanza kwa kituo hicho
kutengeneza jiko linalotumia nguvu ya jua moja kwa moja.
“Hivi sasa tunafanya utafiti kama
tunaweza kulitengeneza dogo lakini lenye nguvu au kutengeneza jiko
linaloweza kukunjwa na kuhifadhiwa kirahisi kwa sababu hili ni kubwa na
inakuwa shida ikiwa mtu hana nafasi kubwa ya kuhifadhia,” anasema
Mhandisi Noela.
Akizungumzia kuhusu ufanisi wake,
Noela anasema kwamba, jiko hilo ni rafiki mkubwa wa mazingira na lina
uwezo mkubwa wa kupika na hata kuoka vyakula vya aina zote ikiwa tu
kutakuwepo na jua la kutosha.
Kwa maeneo kame na yenye jua kali
kama mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na hata Dar es Salaam,
jiko hilo linafaa sana kutumiwa bila shida, anaongeza mhandisi huyo.
Aidha, anafafanua kwamba, jiko
hilo linaweza kupika chakula kwa ajili ya watu wengi na kwamba ni jukumu
la jamii kugeukia matumizi ya jiko hilo lisilotumia mafuta wala nishati
nyingine kwa sababu siyo tu linapunguza gharama, lakini pia linaokoa
misitu kwa vile miti haitakatwa ikiwa watakuwa wanalitumia.
“Jambo jingine la muhimu ni
kwamba, upikaji kwa kutumia jiko la umeme-jua mara nyingi hufanyika nje
na katika mazingira ambayo yanahitaji matumizi madogo ya mafuta na kuni,
au hatari ya ajali za moto na inaokoa afya za wanajamii, hususan
akinamama pamoja na kuyalinda mazingira yetu,” anaongeza Mhandisi Noela.
“Kama unavyoliona, jiko hili
limetengenezwa kwa vifaa maalum vikiwemo vioo, ambavyo vinang’aa na
kuakisi mwanga wa jua, vimepangwa kitaalam na mwanga huu unapoakisiwa
unakwenda moja kwa moja kwenye sufuria ambayo kutokana na joto lake,
chakula chochote kinachopikwa kinaiva bila wasiwasi wowote. Kama jua
litakuwepo la kutosha, joto linalozalishwa na jiko hili linaweza kufikia
hadi nyuzijoto 400 °C.”
Kwa mujibu wa mhandisi huyo,
vyakula vinavyopikwa kwa kutumia jiko la aina hiyo ni vyema vikawa
katika maumbile madogo ili kusaidia kuiva haraka na kwamba muda wa
chakula kuiva unategemea na vifaa unavyotumia, kiwango cha jua, na kiasi
cha chakula kinachopikwa.
Faida kubwa za utumiaji wa jiko
la umeme-jua zinatajwa kwamba, mbali ya kuokoa mazingira, ni uwezo wa
kupika vyakula vigumu, kukaanga nyama, kupika supu, kuoka mikate na
kuchemsha maji kwa muda mfupi.
Hata hivyo, jiko hilo linahitaji zaidi uwepo wa jua, kwani ndiyo chanzo cha joto linalofaa kupikia.
Mmoja wa wanakikundi hicho,
Esther Moshi, amesema kupatikana kwa jiko hilo kutawakomboa wanawake
wengi ambao mara nyingi ndio wanaokabiliwa na changamoto ya utafutaji wa
nishati za kupikia kama kuni na mkaa.
“Tunashukuru mradi wa Green
Voices kwa sababu unalenga kumkomboa mwanamke kutokana na adha ya
upatikanaji wa nishati ya kupikia, kama majiko haya yatatengenezwa kwa
wingi na kila familia kulipata, hakika yatakuwa mkombozi na yatasaidia
kuokoa mazingira, ” anasema.
Fatima Aziz Faraji ni mwenyekiti
wa Chama cha TAWOCA, amesema ni muhimu kwa wanawake kuzidisha umoja wa
vikundi ili waweze kusonga mbele na akaupongeza mradi huo kwamba utakuwa
mkombozi si kwa wanawake pekee, bali jamii nzima.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa
jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi,
ameupongeza mradi wa Green Voices pamoja na akinamama hao na akahimiza
kuwa, ni vyema kutumia teknolojia ambazo ni rafiki wa mazingira.
Amesema akinamama ndio waathirika
wakubwa wa matumizi ya nishati za kupikia, na kwamba ndio wanaoongoza
kupata madhara kiafya, hasa wanapotumia mkaa na kuni.
“Jitihada hizi za wenzetu wa
Green Voices zinapaswa kuongezwa, kwa sababu zinalengo siyo tu kumkomboa
mwanamke, bali kulinda mazingira yetu ambayo yanazidi kuteketea kila
uchao kutokana na ukataji wa misitu kwa madhumuni ya kutafuta kuni na
mkaa.
“Akinamama wanaathirika sana,
wengine utakuta macho mekundu kutokana na moshi wa kuni, na wanapokuwa
wazee ndio wanaoshambuliwa na watu wengine wasio na utu kwamba eti ni
wachawi kwa sababu macho yao ni mekundu, lazima kutumia teknolojia
mbadala kuwanusuru mama zetu, ” alisema.
Hata hivyo, aliwataka akinamama hao kushikamana pamoja katika shughuli zao ili waweze kujiletea maendeleo, kwani umoja ni nguvu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi
wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, amesema, mradi wa
jiko la umeme-jua ni sehemu ya miradi 10 inayotekelezwa chini ya Green
Voices ambapo Tanzania ndiyo pekee iliyopendekezwa kutekeleza mradi huo
unaofadhiliwa na Taasisi ya Mfuko wa Wanawake wa Afrika, , ambayo
inaongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa
Fernandez de la Vega Sanz.
Hata hivyo, taasisi hiyo
inafadhili miradi 15 ya wanawake katika nchi 12 barani Afrika ambayo
imeonyesha mafanikio, huku mradi wa Green Voices ukitajwa kuwa na
mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
Kwa mujibu wa Bi. Secelela, Mradi
wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa sita ya Tanzania Bara ambayo
ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro.
“Miradi hiyo ni kilimo cha miti
ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani Ukerewe mkoani
Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa mbogamboga
kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula
mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga,
na kilimo cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani
Pwani na mradi huu wa utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani
Kilimanjaro,” anafafanua Secelela.
Anasema, lengo kubwa la mradi wa
Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa kupambana
na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya kitanzania iweze
kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko
ya tabianchi.
Serikali kupitia taasisi na idara
zake zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya
Maendeleo ya Jamii imekuwa ikiendesha program mbalimbali za mafunzo ya
ufundi ikiwemo utengenezaji wa majiko banifu na sanifu kama inayoendelea
katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Malampaka wilayani Maswa.
Hata hivyo, bajeti ndogo imekuwa changamoto kubwa kukwamisha kuwafikia wananchi wengi na kuwapatia elimu ya aina hiyo.
No comments:
Post a Comment