Serikali kupitia Wizara ya
Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi wa uamuzi wake wa kuzuia biashara
ya usafirishaji wa wanyamahai nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu
mfululizo na kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa lengo la kupanga
vizuri biashara hiyo kwa faida ya serikali na wafanyabiashara wenyewe.
Ufafanuzi huo umetolewa jana na
Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne Maghembe katika kikao
alichokiitisha wizarani hapo na wafanyabiashara wa wanyamahai wa makundi
ya wadudu, vyura, mijusi, ndege, nyani na tumbili ambao walitaka kupata
ufafanuzi wa hatima ya biashara yao kutoka serikalini.
Katika risala iliyosomwa na
kiongozi wa wafanyabiashara hao, Adam Rashid Warioba kwa Waziri
Maghembe, aliiomba Serikali kutoa ufafanuzi wa hatma ya biashara yao
iliyofungiwa ambayo imekuwa tegemeo pekee katika kuendesha maisha yao
huku wakitaka kujua hatma ya wanyamahai waliohifadhiwa na gharama zao
walizolipia Serikalini.
Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa
Serikali kufungia biashara hiyo kwa wafanyabiashara hao, Prof. Maghembe
amesema wanyamahai wengi kutoka nchini Tanzania wamekuwa wakisafirishwa
nje ya nchi bila ya kufuata utaratibu maalum ikiwemo vibali vya kukamata
na kuwasafirisha wanyama hao jambo ambalo limekuwa likiikosesha
serikali mapato mengi.
“Wapo kati yenu ambao walikuwa
wanasafirisha wanyamahai kinyume cha sheria, bila vibali vyovyote, na
wanyama wa Tanzania walikuwa wakimatwa kwenye bandari na viwanja vya
ndege, ambao wanasafirishwa kinyume cha sheria, wengi tu, na ndio maana
Serikali ikasema hii biashara tusimamae kwanza tuwekwe utaratibu ambao
kila mtu ataufuata, na ambao hautaweza kututia aibu huko nje” alisema.
Alisema sababu nyingine
iliyopelekea serikali kufunga biashara hiyo kwa muda ni bei ndogo
inayouzwa wanyama hao nje ya nchi ambayo haiwanufaishi wafanyabiashara
na Serikali ukilinganisha na thamani yake kwa kile wanachoenda
kufanyiwa, alitolea mfano tumbili ambao hufanyiwa utafiti wa madawa
mbali mbali na baadae kuuzwa mabilioni ya fedha huku tumbili huyo
akiuzwa kwa dola 25 tu.
“Nimefurahi yule bwana aliyesema tumbili mmoja ni dola 25, lakini akasema hao ndio wanafanya medical research (utafiti wa madawa) yote duniani, sasa sisi tunapata dola 25 na wenzetu wanafanya research (utafiti) wanatuuzia madawa yote billions of dollars
(mabilioni ya dola za kimarekani), tuweke utaratibu na ninyi
mtakapokuwa mnafanya hii biashara mpate sio lazima serikali ndio lazma
ipate, mpate kilicho sawa na thamani ya wanyama mnaowauza”, alisema
Prof. Maghembe.
Aliwahakikishia wafanyabiashara
hao kuwa Serikali ya awamu ya tano ni sikivu hivyo kuahidi kushuulikia
changamoto walizoziwasilisha hadi kufikia Januari 10, mwakani (2017),
aliwaeleza kuwa hatma ya wanyamahai ambao wamewahifadhi pamoja gharama
za vibali walizowalipia serikalini zitashuulikiwa.
“Ambacho ninaweza kuwaambia hapa
leo, kwamba tumepata hii taarifa, tunayo ile idadi ambayo imepitiwa na
wataalamu huko kwenye mazizi, tunazo zile permit (vibali) za
serikali ambazo mmepewa na leseni, vyote vile mlivyonavyo na sisi
tunavyo, tutavipitia vyooote kabisa, alafu tutaona ni namna gani
tutawainua kwa kuwafuta jasho”, alisema.
Aliongeza kuwa “Tutaangalia kila
mfanyabiashara ameilipa nini serikali, kwa wanyama hawa ambao wapo,
ambao katazo lilipofanywa walikuwa nao kwenye mazizi yao na wanyama hao
tunawafanyia tathmini tukishakamilisha tutaamua sasa wanyama hao
wanapelekwa wapi, na maeneo yenyewe ni machache tu, ama kwenye mazoo,
ili waweze kutunzwa na kuendelezwa kwa vile ni vigumu kuwarudisha tena
maporini.
“Na kutokana na vibali na risiti
mbalimbali ambazo wameilipa serikali katika kuwapata hao wanyama basi
tutaviangalia na kuangalia utaratibu wa kuwarudishia wale
wafanyabiashara hela zao”.
Akizungumzia lalamiko la
wafanyabiashara hao kuwa wao wamezuiliwa kufanya biashara hiyo huku
mfanyabiashara mmoja kutoka nje akiruhusiwa kufanya biashara hiyo kwa
tangazo la serikali, Prof. Maghembe anasema “Na hilo tangazo mnalosema
lina mtu amebebwa hamna ruhusa ya mtu kubebwa hapa, na mtu atayempa huyo
mtu kibali mnafahamu kitakachotokea, hakuna ruhusu, ndivyo serikali
ilivyosema”.
Mei 26, mwaka huu, akifanya
majumuisho ya hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake
kwa mwaka 2016/17, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne
Maghembe, alitangaza kuwa ni marufuku kusafirisha wanyamahai wote nje ya
nchi kwa miaka mitatu mfululizo.
“Kuanzia sasa (saa moja na dakika
tano usiku) kwa miaka mitatu serikali imepiga marufuku usafirishaji wa
wanyamahai wote kwenda nje ya nchi, hata chawa wa Tanzania
hawataruhusiwa kusafirishwa nje, Na katika kipindi hiki cha miaka
mitatu, idara ya wanyamapori itafanya kazi ya kuishauri serikali namna
gani biashara hiyo itakavyoendeshwa”, alisema Prof. Maghembe.
Imetolewa na;
Hamza Temba
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii
No comments:
Post a Comment