• Breaking News

    ..

    ..

    Friday, 20 January 2017

    MHE. MHAGAMA ASHAURI CHAMA CHA AKIBA NA MIKOPO OFISI YA WAZIRI MKUU (MAKAMU SACCOS) KUWA WABUNIFU

    Na mwandishi wetu.
    Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama ameshauri uongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Ofisi ya Waziri Mkuu (Makamu Saccos) kuwa na ubunifu katika utendaji ili kuleta manufaa zaidi kwa wanachama wake.

    Mhe. Mhagama ameyasema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanachama wa Chama hicho uliofanyika Januari 19, 2017 mkoani Dodoma.

    Katika Mkutano huo Mhe. Waziri alisisitiza kuwepo na mikakati madhubuti ya kubuni miradi itakayowezesha chama kuwa na vyanzo vyake vya mapato na kuwa na mikakati ya kuongeza wanachama wapya kwa kuzingatia umuhimu wa chama hicho.
    “Ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kubuni miradi, kuongeza wanachama pamoja na kuwa na vitu vya kiupekee na vya kiufanisi vitakavyokisaidia chama kuwa imara katika utendaji wake”, alisema Waziri Mhagama.

    Aliongeza kuwa chama hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake amabapo wengi wao wamekuwa na maendeleo mbalimbali kutokana na uwepo wa fursa za mikopo isiyokuwa na masharti magumu.

    “Chama kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wanachama wake kwani wamekuwa wakikopa na kusaidia katika shughuli za kimaendele, ikumbukwe kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi wana maendeleo kwakuwa wanachukua mikopo mbalimbali inayowasaidia kuwepo na maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja”, alisisitiza Mhe.Mhagama.

    Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Joseph Muhamba aliahidi kuyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa na Mhe.Waziri na kuyaweka katika vitendo ili kuhakikisha chama kinaongeza mbinu za ubunifu ikiwemo eneo la kuongeza wanachama wapya na kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wanachama waliopo.

    Mhe. Mhagama aliahidi kutoa ushirikiano wake kwa Chama hicho na kueleza kuwa chama kiitumie fursa ya Serikali kuhamia Dodoma kama chachu ya kuongeza wanachama wapya.

     “Ninawaahidi kuwapa ushirikiano wa hali na mali na kuamini kuwa chama hiki ni msaada mkubwa kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwani kipo kisheria kabisa na zipo kanuni zinazoelekeza juu ya uwepo wa chama na kwa kuonesha mfano mimi na Naibu Waziri Mhe. Dkt. Possi tunajiunga rasmi hii leo ili kuwa mstari wa mbele kukisaidia chama hiki”. Alisema Mhe. Mhagama.

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI