• Breaking News

    ..

    ..

    Saturday, 18 February 2017

    SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKIANO NA WAFANYABIASHARA ILI KUKUZA UCHUMI WA NCHI

    mb2
    Naibu Kamishna wa TRA, Bw. Qandiyay Akonaay, akitoa maelezo namna Idara ya Forodha inavyotekeleza majukumu yake katika Mpaka wa Kasumulu/Songwe (Tanzania na Malawi) baada ya kutembelewa na Ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ukiwahusisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya.
    mb03
    Baadhi ya maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji, na Mamlaka ya mapato Tanzania TRA, wakifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa wakati wa ziara ya ujumbe wa Serikali ukihusisha Makatibu wakuu wa Wizara hizo na Taasisi zake, walipotembelea na kukagua shughuli za forodha na uhamiaji zinazoendelea katika mpaka huo wa Tanzania na Malawi, eneo la Kasumulu.
    mb3
    Afisa Forodha  wa mpaka wa Tanzania na Malawi Mkoani Mbeya-Kasumulu, Bw. Lenny Mkolla (Wa nne kulia) akitoa maelezo kuhusu mpaka huo baada ya kutembelewa na  Ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban (wa pili kulia), Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda (wa tatu kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya (hayupo pichani), Wilayani Kyela Mkoani Mbeya.
    mb4
    Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya (wa kwanza kulia), akitoa ushauri kwa uongozi wa mpaka wa Kasumulu/Songwe (Tanzania na Malawi), upande wa Tanzania, Wilayni Kyela Mkoani Mbeya, namna ya kuboresha utendaji kazi mpakani hapo ili kuboresha biashara na kuongeza   mapato ya Serikali. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda (wa pili kulia), Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji-Kasumulu, Bw. John Gillagiza (wa kwanza kushoto), walipotembelea mpaka huo..
    mb5
    Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akisisitiza kauli mbiu ya “siku moja! mzigo umetoka” kwa watumishi wa Idara ya Forodha katika mpaka wa Kasumulu/Songwe (Tanzania na Malawi), baada ya ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban (kulia) ulipotembelea na kukagua mpaka huo wilayani Kyela mkoani Mbeya.
    mb7
    Mfanyabiashara ndogo ndogo katika Mpaka wa Kasumulu/Songwe (Tanzania na Malawi, wilayani Kyela mkoani Mbeya, Bw. Maombi Simon, akiwa anafuatilia ziara ya Ujumbe wa Serikali kutoka Wizara tatu za Fedha, Uwekezaji na Mambo ya ndani, uliotembelea mpaka huo kukagua shughuli za idara ya Forodha na Uhamiaji, mpakani hapo.
    mb1
    Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (wa kwanza kushoto), Naibu Kamishna wa TRA, Bw. Qandiyay Akonaay (wa pili kushoto), na wajumbe wengine wakiwasili katika Ofisi za Idara ya Uhamiaji katika Mpaka wa Kasumulu/Songwe, (Tanzania na Malawi), ili kukagua shughuli za forodha katika mpaka huo, wilayani Kyela Mkoani Mbeya.
    (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
    ……………………………………………………………………………
    Benny Mwaipaja-WFM, Kyela
    KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa sekta ya biashara katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi hivyo itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na uwekezaji.
    Prof. Mkenda amesema hayo wilayani Kyela Mkoani Mbeya, wakati ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, ulipotembelea mpaka wa Tanzania na Malawi-Kasumulu, ili kujionea utendaji kazi wa Idara ya Forodha na Uhamiaji katika mpaka huo wa Kasumulu/Songwe.
    Amesema kuwa Serikali inapohimiza ulipaji na kusimamia ulipaji kodi haina maana kwamba inawachukia wafanyabiashara, bali inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa na kutoa wito kwa idara za Serikali zilizoko Mipakani kuboresha mazingira ya utoaji huduma ili kurahisisha biashara.
    “Tunatakiwa kuondoa vikwazo vya ufanyaji biashara ikiwemo ucheleweshaji wa mizigo inayovushwa katika mipaka yetu kwa kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuzivutia nchi nyingi zaidi kutumia Bandari hiyo” Aliongeza Profesa Mkenda
    Amewaonya watendaji wa Serikali walioko katika mipaka yote ya nchi, kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kusisitiza kuwa wale wote watakaoshindwa keendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ni afadhali wapishe kwa hiari yao.
    Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, amesema kuwa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifawa miaka Mitano, unahitaji zaidi ya Shilingi Trilioni 107 na kwamba upatikanaji wa fedha hizo utahitaji mazingira bora ya kukuza uchumi wa nchi ikiwemo mazingira mazuri ya ufanyaji biashara mipakani
    “Serikali itazifanyiakazi changamoto mlizozisema kama vile upungufu wa wafanyakazi, vitendeakazi na nyumba za watumishi, lakini wito wangu kwenu muendelee kufanyakazi kwa pamoja, mshirikiane kwa kuongeza nguvu ili kuongeza mapato ya Serikali” alisisitiza Bi. Amina Khmis Shaaban
    Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi, Balozi Hassan Simba Yahya, amelitaka jeshi la polisi hususan kikosi cha usalama barabarani kupunguza urasimu wakati wa kutekeleza majukumu yao wanapokutana na magari yaendayo masafa marefu nje ya mipaka ya Tanzania, wasiyacheleweshe njiani bila sababu za msingi.
    Kwa upande mwingine, Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Qandiyay Akonaay, ameeleza kuwa TRA imeanzisha mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mizigo inayosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwenda nchi jirani, hatua ambayo imeboresha kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa mizigo na kwamba hatua hiyo pia imeongeza mapato ya kodi ya Serikali

    No comments:

    Post a Comment

    HABARI

    HABARI

    MICHEZO

    LOGO

    LOGO

    MAOJIANO

    BURUDANI